Drawer trigger

Uislamu Chaguo Langu 21 + Sauti

Sikiliza Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika katika kipindi hiki maalumu kuhusu watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina wameamua kusilimu na kuikumbatia dini tukufu ya Kiislamu. Katika makala ya leo tutamuangazia Mmarekani aliyesilimu Diana Beatty. Karibuni kujiunga nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Nafasi ya hekima katika mafundisho ya Kiislamu iko wazi kabisa. Qur'ani Tukufu kwa mara kadhaa imetoa wito kwa wanaadamu kuchunguza kwa hekima na kwa mantiki mafundisho ya kidini na wala wasikubali ulazimishaji na uigaji kibubusa. Katika Qur'ani Tukufu aya za 17 na 18 za Sura Azzumar Allah SWT anasema: "Na wale wanaojiepusha na ibada potovu, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu. Ambao husikiliza maneno, wakafuata lilio bora yao. Hao ndio alio waongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili." Vile vile katika sehemu ya aya ya 256 ya Surat al Baqara tunasoma hivi: "Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu." Lakini katika Ukristo ulioko sasa duniani tunashuhudia kuwepo mgongano mkubwa kutokana na itikadi potofu ya utatu na kumtaja Nabii Issa AS kuwa ni mungu. Suala hilo limepelekea Wakristo wengi kutoweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu. Profesa Mohammad Legenhausen mmoja kati ya watafiti wa Kiislamu kutoka Marekani ambaye binafsi alisilimu mwaka 1983 baada ya kuutambua uhakika anasema hivi: "Kile ambacho kilinivutia zaidi ya yote katika Uislamu ni kiasi kikubwa ambacho dini hii inawahimiza wanaadamu kuuliza maswali na kuendelea kuwataka wafanye utafiti zaidi kuhusu mafundisho ya kidini." Diana Beatty Mmarekani aliyesilimu ambaye amechagua jina la Masooma anasema hivi kuhusu uamuzi wake wa kuikumbatia dini tukufu ya Kiislamu: "Mimi nilizaliwa katika jimbo la Colorado katika familia ya Kikristo ambayo haikuwa imefungamana sana na mafundisho ya Kikristo. Kwa hakika Ukristo haukuwa na nafasi katika familia yetu. Baba yangu alikuwa na itikadi za Mormon ambalo ni pote katika Ukristo na mama yangu alilelewa katika familia ya Kiprotestanti. Nakumbuka kuwa ilipokuwa ikifika siku ya Jumapili wazazi wangu walikuwa wakinichukua mimi na kaka yangu na kutupeleka katika shule ya kidini. Wao hawakuwa wakienda kanisani bali walikuwa wakibaki nyumbani. Nilipofika katika umri wa ubarobaro nilianza kufanya utafiti kuhusu kumjua Mwenyezi Mungu. Nilikuwa nakijiuliza: "Je, kweli Mwenyezi Mungu yupo na iwapo yupo anataraji nini kutoka kwetu sisi kama wanaadamu? Nilianza kuchunguza Bibilia na vitabu vingine  vya Kikristo na kuvisoma bila mapendeleo.  Wakati nilipokuwa nikisoma katika shule ya upili niligundua kuwepo migongano katika Bibilia. Katika Injili Nabii Issa AS alikuwa akitajwa kama mungu na sehemu nyingine kama mwanaadamu. Nilikuwa nikifikiri kuwa tatizo la ufahamu ni langu binfasi kutokana na kutokuwa na uwezo wa kudiriki maudhui ipasavyo." Bi. Maasooma anaendelea kufafanua kuhusu alivyoikumbatia dini tukufu ya Kiislamu kwa kusema: "Daima nimekuwa nikivutiwa na tamaduni tafauti. Hatua kwa hatua maswali kuhusu Uislamu yalianza kunijia akilini. Katika siku hizo nilizokuwa nikifanya utafiti nilipata fursa na kujuana na Mwislamu mmoja. Nilianza kujiuliza: "Je, ni kwa nini anaswali kwa njia hii maalumu?  Nilikuwa nikitaka sana kujua ni kwa nini anafungamana sana na itikadi pamoja na amali zake. Ukristo hauna njia maalumu ya kufanya ibada. Katika Ukristo nilifunzwa kuwa kila chochote nilichotaka ningemuomba Nabii Issa na wala si Mungu. Katika Ukristo hakuna ufahamu wa ibada halisi. Mimi nilikuwa na hamu kubwa ya kujua uhusiano wangu na Mungu kabla ya kuomba dua. Ni kwa sababu hii ndio niliamua kuisoma Qur'ani Tukufu kupitia tarjumi yake ya Kiingereza. Mara ya kwanza niliposoma Qur'ani, nilikuwa na mitazamo miwili tafauti. Kwa upande mmoja nilishangaa kuona visa vya mitume wengi wa Kikristo na Uyahudi katika Qur'ani. Kabla ya hapo sikuwa nikifahamu chochote kuhusu uhusiano wa Ukristo, Uyahudi na Uislamu. Nilikuwa na dhana potofu kuwa Uislamu ni sawa na dini za Mashariki kama vile Ubudha. Kwa upande mwingine niliifunga Qur'ani niliposoma aya zake zisemazo kuwa Nabii Issa AS si mungu kama nilivyokuwa nimefundishwa katika itikadi ya Utatu ya Ukristo. Hii ni kwa sababu niliyokuwa nimeyasikia yalikuwa kinyume kabisa na yale yaliyomo katika Qur'ani. Pamoja na hayo kadiri nilivyoendelea kusoma Qur'ani Tukufu niliona mafundisho yake yanaenda sambamba na imani yangu ya dhati na hapo nilijuta ni kwa nini nilikubali kwa urahisi mafundisho ya Kikristo," anasema Mmarekani aliyesilimu Bi Maasouma Beatty. Katika dini tukufu ya Kiislamu suala la kutumia mantiki limepewa umuhimu mkubwa. Aya 256 za Qur'ani zimezungumzia suala la kutumia akili na kutafakari. Kwa hakika mafundisho yote ya Kiislamu yanaenda sambamba na akili pamoja na mantiki. Bi.Maasouma Beatty katika utafiti wake kuhusu Uislamu alijitahidi kutumia mantiki na akili kufikia ukweli. Mwanzoni mwa utafiti wake hakuwa anajua mengi kuhusu Uislamu. Aghalabu alikuwa akiisoma Qur'ani iliyotarjumiwa kwa Kiingereza na kutafakari kuhusu aliyoyasoma. Alikuwa akilinganisha mafundisho ya Uislamu na Ukristo ili kufikia ukweli. Bi Beatty alikuwa akiwauliza maswali Wakristo waliokuwa wakisoma Injili kwa kina lakini hawakuwa wakimpa majibu sahihi. Anasema: "Kwa mfano katika Injili hakuna sehemu yoyote iliyoandikwa kuwa Nabii Issa AS ni mungu katika muundo wa mwanaadamu wala hakuna sehemu yoyote iliyosema kuwa ni sharti kuamini kuwa yeye ni mwana wa Mungu. Wakristo wanasema haya ni mambo unayopaswa kuyakubali moyoni na haipaswi kuuliza maswali. Lakini mimi niliwaza na kutafakari kuwa iwapo Mwenyezi Mungu ametupa dini basi inapaswa kuenda sambamba na mantiki na akili ili tuweze kuifahamu na hatimaye tutende amali zetu kwa mujibu wa ayatakayo Mwenyezi Mungu. Mkuu wa kundi moja la wasoma Injili alikuwa ameenda Algeria kuhubiri Ukristo. Niliamua kumuuliza maswali kwani nilidhani kuwa anaufahamu Uislamu kwa kiasi fulani na hivyo anaweza kuashiria dosari katika Uislamu na faida za Ukristo. Awali nilimuuliza, je, umeshaisoma Qur'ani. Nilishangazwa na jibu lake kwani alisema amewahi kuipitia juu juu. Nilifikia natija kuwa kutokana na kuwa nimeisoma Qur'ani kwa miezi kadhaa na naufahamu Uislamu zaidi ya mhubiri huyo Mkristo niliamua kukata uhusiano wangu naye. Nilisema kuwa mtu ambaye hajaisoma Qur'ani hawezi kamwe kutoa maoni kuhusu kitabu hicho kitakatifu. Nilikasirishwa sana naye pamoja na viongozi wote wa Kikristo ambao huzungumza kuhusu Uislamu bila kuusoma. Nilifikia natija kuwa kile wahubiri Wakristo wanachofunza ni mitazamo yao tu huku wakidai ni itikadi ya Mwenyezi Mungu. Tukio hilo lilipelekea mitazamo yangu ibadilike kabisa kwani nilifikia natija kuwa siwezi kumtegemea mtu katika utafiti niliokuwa nikifanya bali nilipaswa kufanya utafiti peke yangu.  Hatua kwa hatua nilifikia natija kuwa sikuwa naamini tena itikadi ya utatu. Sikuweza tena kupinga kuwa Mohammad SAW ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Qur'ani ni neno la Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo baada ya miezi michache niliikumbatia dini tukufu ya Kiislamu." Katika ulimwengu wa Magharibi kunaenezwa propaganda kuwa katika Uislamu nafasi ya mwanamke ni dhaifu na kwamba amenyimwa haki na kutengwa. Lakini wanawake ambao wameamua kuukumbatia Uislamu si tu kuwa wanaamini propaganda hizi ni potofu bali pia wanasema moja ya sababu za kusilimu kwao ni suala la kuzingatiwa mwanamke katika Uislamu na kupewa haki na hadhi ya juu. Bi. Maasouma Beatty anasema hivi kuhusu suala hili: "Uislamu umepelekea nistawi kama mwanamke. Nimeona wanaume wengi Waislamu ambao wanamheshimu sana mwanamke kuliko inavyoshuhudiwa katika jamii ya Marekani. Hivi sasa ninafurahi sana kutokana na kuwa mimi ni mwanamke Mwislamu. Kabla ya kusilimu nilikuwa nikichukia kuwa mwanamke kwani niliamini kuwa iwapo ningelikuwa mwanaume ningeweza kuishi kwa njia sahali zaidi. Lakini sasa nikiwa mwanamke Mwislamu nahisi nina hadhi ya juu. Ninapenda kuwa mwanamke." Bi. Masooma Beatty anasimulia kumbukumbu ifuatayo kuhusu namna alivyoamua kuvaa Hijabu pamoja na kuwepo vizingiti vingi dhidi ya vazi hilo Marekani: "Baada ya kuvaa Hijabu nilipata hisia nzuri sana na kwa kweli nilihisi kuwa mimi ni mwanamke kamili. Nilihisi kuwa nimepata rehma na msaada wa Mwenyezi Mungu nikiwa nimevaa Hijabu kuliko wakati ambao sikuwa na vazi hili la stara. Baadhi ya marafiki zangu wa chuo kikuu hata walifurahishwa na Hijabu yangu." Wapenzi wasikilizaji Uislamu uliibua mabadiliko makubwa katika maisha ya Maasouma na sasa anajitahidi kueneza mabadiliko hayo ya kimaanawi kwa wengine ili waweze kuifahamu na kuifuata dini tukufu ya Kiislamu. Ni kwa sababu hii ndio ameandika kitabu chenye anwani ya Seeking the Straight Path: Reflections of a New Muslim yaani Kutafuta Njia ya Haki: Mtazamo wa Aliyesilimu, ili wengine waweze kufaidika na kisa cha mabadiliko katika maisha yake. http://kiswahili.irib.ir