KUBADILISHWA KIBLA

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

Kubadilishwa kibla cha Waislamu kutoka Beitul Muqaddas kuelekea Makka. Katika kipindi cha miaka 13 ya kubaathiwa na Mwenyezi Mungu mjini Makka na miezi kadhaa tokea ahajiri mjini Madina, Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akifanya ibada zake pamoja na wafuasi wake wakiwa wameelekea Beitul Muqaddas. Hili ni eneo ambalo alizaliwa Nabii Isah (as) na kituo muhimu cha Mayahudi na Wakristo. Hii ni katika hali ambayo watu wa Makka katika zama hizo waliipa Kaaba umuhimu mkubwa na kuifanya kuwa kituo cha kuabudia masanamu yao.

Lakini wakati Mtume Mtukufu (saw), alipowasili mjini Madina na kuanza kutekeleza ibada zake akiwa ameelekea upande wa Beitul Muqaddas, Mayahudi waliokuwa wakiishi mjini hapo walianza kulalamika na kueneza propaganda nyingi dhidi ya Waislamu wakidai kwamba hatua yao hiyo ilikuwa ni dalili ya wazi ya kuthibitisha kwamba hawakuwa huru wala kujitawala na kwamba jambo hilo lilithibitisha kuwa Mayahudi ndio waliokuwa kwenye njia sahihi na ya haki. Jambo hilo lilichukuliwa na Mayahudi kuwa kisingizio kizuri cha kuwakejeli na kuwaudhi Waislamu wakiongozwa na Mtume Muhammad (saw).

Jambo hilo lilikuwa likimuudhi sana Mtume na akikesha kufanya ibada na kusubiri wahyi wa Mwenyezi Mungu uteremke ili umfariji kuhusiana na suala hilo. Hatimaye siku moja, Mtume alipokuwa amemaliza rakaa ya pili ya swala ya Adhuhuri, Mwenyezi Mungu alimuamuru Malaika Jibril (as) amteremshie Mtume wahyi. Akiwa katika hali hiyo ya swala, Malaika Jibril aliteremka na kuushika mkono wa Mtume na kisha kumuelekeza upande wa Makka: "Kwa yakini tukiona unavyogeugeuza uso wako mbinguni. Basi tutakugeuza kwenye Kibla ukipendacho. Basi geuza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu (al-Kaaba); na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu uliko (msikiti huo); na hakika wale waliopewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao; na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda (Baqarah:144).

Bada ya kutimia amri hiyo ya Mwenyezi Mungu, Mayahudi walikasirishwa sana na kuatumia mbinu nyingine ya kueneza propaganda sumu dhidi ya Mtume (saw) na wafuasi wake. Walianza kuhoji ni kwa nini Waislamu waliacha kuelekea kwenye kibla cha kale cha Manabii waliotangulia wa Mwenyezi Mungu? Walisema, ima ibada yao ya zamani ilikuwa batili au kitendo chao hicho cha kubadili kibla kilikuwa na kasoro. Katika aya iliyotajwa, Mwenyezi Mungu anawajibu Mayahudi hao kwa kuwaambia kuwa sehemu zote ni Zake Yeye na kwamba waja wake wanapasa kuswali na kutekeleza ibada zao wakiwa wameelekea katika kila sehemu Anayoamrisha Yeye. Mwenyezi Mungu anasisitiza kwamba sehemu yoyote ile haina utukufu wa dhati isipokuwa baada ya kupewa utukufu huo na Yeye mwenyewe: "Karibuni wapumbavu miongoni mwa watu watasema; Nini kilichowageuza kutoka kibla chao walichokuwa wakikielekea? Sema (Uwaambie): Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; humuongoza amtakae kwenye njia iliyonyooka (Bagara:142)."

Falsafa ya kubadilishwa kibla

Kwa mujibu wa nyaraka za Kiislamu, inaonekana kuwa kubadilishwa kibla cha kwanza cha Waislamu kulitokana na sababu kadhaa zikiwemo zifuatazo: Wakati Mtume Mtukufu (saw) alipokuwa katika mji mtakatifu wa Makka ambapo washirikina walikuwa wakiipa al-Kaaba umuhimu mkubwa, mtukufu huyo alihisi kuwepo haja ya kutofautishwa safu za Waislamu na washirikina hao na kwa hivyo wakabadilishiwa kibla chao kueekea Beitul Muqaddas. Lakini baada ya kuhajiri na kuja Madina, licha ya kuwa katika hatua ya mwanzo Waislamu walikuwa wakiswali na kutekeleza ibada zao wakiwa wameelekeza nyuso zao hukohuko Beitul Muqaddas, lakini ni dhahiri kuwa walikuwa na hamu kubwa ya kutaka kubadilishwa kibla hicho kutokana na kejeli pamoja na udhia waliokuwa wakiupata kutoka kwa Mayahudi kuhusiana na jambo hilo. Hii ni katika hali ambayo Mayahudi na Wakristo tayari walikuwa na habari ya kuja Mtume ambaye angeswali kuelekea kibla mbili, kutokana na yale waliyokuwa wakiyasoma kwenye vitabu vyao vya kidini. Hilo pia ni jambo ambalo limebainishwa wazi katika Qur'ani tukufu.

Kuwajaribu Waislamu ambao bado walikuwa na athari za kipindi cha ushirikina na ukafiri na hawakuwa wamefikia daraja ya kusilimu kweli. Watu kama hao waliichukulia amri ya kubadilishwa kibla kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa jambo gumu kwao na Qur'ani pia imeashiria wazi jambo hilo: "….Na hatukukifanya kibla ulichokuwa nacho (mara ya kwanza kuwa ndiyo kibla chako sasa na mpaka siku ya mwisho wa ulimwengu) ila tupate kumjulisha (atambulikane) yule anayemfuata Mtume na yule anayegeuka akarejea nyuma. Kwa yakini lilikuwa jambo gumu isipokuwa kwa wale aliowaongoza Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu kwa watu ni Mpole sana na Mrehemevu (Baqarah:143).

IMEANDIKWA NA:   BARAZA