Makala Maalumu kwa Mnasaba wa Maulidi ya Mtume SAW
Makala Maalumu kwa Mnasaba wa Maulidi ya Mtume SAW
0 Vote
88 View
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulidi ya Mtume wetu Muhammad SAW, mbora wa viumbe na rehma kwa walimwengu wote. Ni matumaini yangu kwamba mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Katika kipindi hiki wapenzi wasikilizaji, tumo katika siku za kuadhimisha na kukumbuka tukio kubwa zaidi katika historia ya mwanadamu yaani siku ya kuzaliwa mbora wa viumbe Muhammad bin Abdullah SAW, Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu aliyekuja kukamilisha waliyokuja nayo Mitume wote wa kabla yake kama Ibrahim, Nuh, Mussa na Issa SA. Kwa mnasaba huu adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu bali wanadamu wote ambao Nabii Muhammad alikuja kuwaongoza na kuwaelekeza katika njia nyoofu. Siku aliyozaliwa Nabii Muhammad SAW inakumbusha baraka na rehma zisizo na kikomo za johari hiyo ya ulimwengu katika maisha ya mwanadamu. Tunaweza kusema hapa kuwa hadiya kubwa zaidi ya maulidi na kuzaliwa kwa mtukufu huyo ni tauhidi kwa maana ya itikadi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na uadilifu. Muhammad SAW alikuwa kama upepo mwanana wa kipindi cha machipuo uliofukiza uturi wa tauhidi katika maisha yasiyokuwa na roho ya watu wa zama hizo na kuhuisha tena roho za wanadamu. Muda mfupi baada ya kubaathiwa, mtukufu huyo aliondoa ada na itikadi za kijahilia na taasubi za kikabila na kuwafungulia wanadamu dirisha la maarifa ya ulimwengu wa akhera. Aya ya 157 ya Suratul A'raf inasema kuhusu kazi kubwa aliyoifanya Mtume Muhammad SAW kwamba: "Ambao wanamfuata huyo Mtume, Nabii asiyesoma wala kuandika, wanayemkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anayewaamrisha mema na kuwakataza maovu, na anawahalalishia vizuri na anawaharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao..." Naam, Nabii Muhammad SAW alikuja kuwaondoa wanadamu katika minyororo ya ujinga, dhulma, ukatili na ada mbaya za kikaumu na kikabila. Japokuwa hii leo wanadamu wanaishi katika zama za maendeleo ya kustaajabisha ya sayansi na teknolojia, lakini inasikitisha kuwa bado kiumbe huyo anasumbuliwa na dhulma, ukatili, ada na mila za kijahilia na sheria zinazoshabihiana na zile za enzi za mawe. Mwanadamu wa leo amezama katika umaada uliogubika na kufunika kabisa masuala ya kimaanawi na kiroho, suala ambalo haliwezi kuondolewa bila ya kuhuishwa tena mafundisho adhimu ya Nabii Muhammad SAW ambaye hii leo tunaadhimisha na kusherehekea tukio la kuzaliwa kwake. Zaidi ya miaka 1400 iliyopita Mtume Muhamamad SAW alifanya mapinduzi makubwa na kuasisi mfumo mpya na wa kudumu kwa ajili ya mwanadamu. Misingi mikuu ya mfumo huo ilikuwa uadilifu, kuondoa dhulma na ubaguzi wa kijamii, mabadiliko makubwa katika tabia na mienendo ya watu na kueneza itikadi ya kumwabudu na kumnyenyekea Mola Mmoja badala ya kuwa mtumwa na mja wa miungu bandia iliyochukua sura tofauti kama masanamu, madikteta na watawala wa kiimla. Kipindi cha miaka kumi ya utawala wa dola la Kiislamu mjini Madina chini ya uongozi wa Nabii Muhammad SAW kilikuwa kipindi bora zaidi cha utawala kuwahi kushuhudiwa na wanadamu. Katika kipindi hicho uliasisiwa utawala wa Kiislamu ambao ulikuwa mfano bora wa utawala wa dini na kigezo cha utawala bora kwa ajili ya zama na kila mahala. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa mapinduzi ya Mtume SAW na mfumo wake mpya wa utawala ulikuwa ramani ya njia kwa ajili ya wanadamu wote wanaotafuta ukamilifu. Mfumo kigezo wa utawala wa Mtukufu Mtume huyo huko Madina ulikuwa na vigezo na sifa nyingi hapa tunaashiria baadhi tu. Kwanza ni imani na kumpenda Mwenyezi Mungu Mrehemevu ambayo ilikita mizizi katika nyoyo za wafuasi wa mtukufu huyo na kuanzisha vuguvugu na harakati kubwa. Mtume wa Mwenyezi Mungu alipandikiza katika nyoyo za Waislamu mbegu ya imani ya tauhidi, kuwa mja wa Mwenyezi Mungu pekee, kuwakataa matwaghuti na miungu bandia na kutonyenyekea na kuwa mtumwa wa yeyote isipokuwa Muumba wa wao. Kigezo na kielelezo cha pili katika mfumo wa utawala wa mtukufu huyo kilikuwa ni uadilifu na usawa. Uadilifu ndio uti wa mgongo wa mafundisho ya Mitume wote wa Mwenyezi Mungu na tarajio la siku nyingi la kiumbe mwanadamu. Uadilifu una maana ya kukipa kila kitu haki yake. Nabii Muhammad alitayarisha mazingira bora na salama kwa ajili ya maisha yaliyotawaliwa na masuala ya kiroho na kulinda utukufu wa mwanadamu kwa kueneza uadilifu katika pande zote za maisha. Katika mfumo wa utawala wa Nabii Muhammad SAW mambo yote yalisimama juu ya msingi wa maarifa, elimu na mwamko. Alitangaza suala la kutafuta elimu na maarifa kuwa ni faradhi na wajibu kwa wanadamu wote na kuwataka Waislamu watafute elimu tangu wanapozaliwa hadi wanapelekwa kaburini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maovu na maafa mengi yanayowapata wanadamu yanatokana na ujinga na ukosefu wa masuala ya kiroho katika jamii ya wanadamu. Moja ya sifa za jamii ya mfumo wa utawala wa Nabii Muhammad mjini Madina ni kuwa huru na kujitegemea, masuala ambayo yaliipa nguvu na uwezo mkubwa wa kujiamulia mambo yake. Mfumo wa kisiasa wa zama za Nabii Muhammad SAW haukuwa tegemezi na wa kufuata sera na siasa za pande nyingine, kwani jamii isiyokuwa huru na isiyojitegemea haiwezi kuchukua maamuzi huru bila ya kutegemea au kufuata amri za upande mwingine. Uchapakazi, harakati na maendeleo endelevu ni sifa nyingine ya utawala kigezo wa serikali ya Mtume Muhammad SAW. Uchapakazi na harakati ilikuwa kiini na msingi katika mfumo huo wa utawala. Mtume Mtukufu daima alikuwa akiwaambia vijana kwamba: Mwenyezi Mungu hampendi kijana anayepitisha umri wake hivi hivi bila ya kujishughulisha na kazi." Katika kipindi chote cha utawala wa miaka kumi ya serikali yake mjini Madina, Mtume SAW alikuwa kijishughulisha na kazi mbalimbali za kuwaamsha wanadamu, kuwaelimisha na kuwaongoza katika njia ya ukamilifu. Alishauriana na watu na kushirikiana nao katika kueneza dini ya Mwenyezi Mungu. Demokrasia ilitekelezwa kwa maana yake halisi katika mfumo wa utawala wa Kiislamu mjini Madina na masuala mengi ambayo yamekuja kutukuzwa karne kadhaa baadaye kama "haki za binadamu", "sawa" na kadhalika vilipata maana yake halisi katika jamii ya Mtume Mtukufu. Istiqama na kusimama ngangari katika kutetea malengo aali ilikuwa miongoni mwa sifa za serikali ya Mtume mjini Madina. Kusimama kidete na imara hulipa taifa izza na heshima mbele ya walimwengu na kutoa tahadhari kwa madhalimu na wachokozi. Imani kubwa ya Mtume na kumpenda Mwenyezi Mungu vilizidisha moyo wa kusimama imara katika njia na malengo aali ya Uislamu. Mtukufu huyo hakutetereka wala kulegeza msimamo mbele ya tufani na matatizo mengi yaliyosababishwa na washirikina dhidi ya mfumo mpya wa uadilifu na tauhidi. Daima Nabii Muhammad SAW alikuwa akisema: Muumini katika tufani ya matukio mbalimbali, huwa mithili ya shuke lililokomaa ambalo wakati linapokabiliana na upepo mkali huinama chini kwenye ardhi, na upepo unaposimama huinuka na kusima tena wima." Mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani Bibi Annemarie Schimmel anasema kuhusu adhama ya kazi kubwa aliyofanya Mtume wa Uislamu kwamba: "Mtume wa Uislamu alikuwa na nafasi ya aina yake katika mabadiliko ya kiroho ya mwanadamu. Alihuisha roho ya mwanadamu badala ya mwili wa kiumbe huyo. Alizikomboa fikra za wanadamu na kuziondoa katika minyororo ya kijahili. Bibi Annemarie Schimmel anaendelea kusema: "Nabii Muhammad aliwafundisha wanadamu jinsi ya kutumia vyema jicho, sikio, elimu na akili na akawapa bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba mwanadamu anaweza kudhibiti jua, mwezi na mbingu. Annemarie Schimmel anamalizia kwa kusema: "Kwa msingi huo kumtukuza kiongozi adhimu kama huyu humpa kila mwanadamu saada na hadhi kubwa." Wapenzi wasikiliza kipindi chetu maalumu kwa ajili ya Maulidi ya Mtume SAW kinaishia hapa kwa leo. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wanadamu wote hususan Waislamu kwa mnasaba huu adhimu wa Maulidi ya mbora wa viumbe Muhammad SAW. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. http://kiswahili.irib.ir