NURU YA RAMADHANI
NURU YA RAMADHANI
0 Vote
282 View
Ule mwezi mtukufu wa Ramadhani umetufikia tena Waislam kote ulimwenguni ni kipindi chetu cha kuzidisha Ibada kwani saumu ni tendo la Ucha mungu. Kula na kunywa kuanzia kurubio la kutoka usiku mkubwa kuingia alfajiri hadi kuchwa kwa jua yaani Magharibi. Mbali ya kuzuiliwa huko na kiamsha tumbo na kupooza koo, lakini pia yapo mambo kadhaa ni halali nayo kwa kuadhimisha na kuitikia wito na amri ya Mola nayo yamekatazwa kwa nyakati za mchana na kuidhinishwa yaendelee nyakati za usiku kwa waliostahiki ikiwemo taratibu za wana ndoa . Yale yote yaliyokuwa haramu khasa , nayo uharamu wake unabaki vilevile na kuyatenda katika mwezi huu mtukufu ni dhambi za hali ya juu zaidi na ni jeuri kwa Muumba. Mwezi huu una siri nyingi kwa wafungao, ikiwemo utengenezaji wa afya zao, maadili yao ya kuishi na utafutaji wao wa ridhiki. Miji na nyumba huwa baridi, magomvi hupungua huruma huzidi na tabia zilizozoweana na baadhi yetu hujikanya sisi wenyewe tuziepuke ili saumu zetu zisibatilike.Pana ucha Mungu huu ambao wenye akili hukimbilia na kuongeza maombi yao kwa M/Mungu , lakini mwezi huu kwa bahati mbaya wapo wanaoupatia faida yake na wapo wataopata khasara muda wote huku wamekaa na njaa ya bure. Kwa kuwa Mola huangalia yale yaliyo nyoyoni mwetu, basi anawajua wale wote wanaomuabudu kwa dhati kwenye ibada hii ya saumu na wale ambao wanawachelea wanaadam kuwanongona. Mola anawatambua pia wale wanaosikitika kwa kufika mwezi huu ambao pato lao la kila siku wanadhani limekosekana kwa mwezi huu kuwa pingamizi kwao. Basi makundi haya mawili katika tunaojiamini kuwa sisi ni waislamu na waumini kila mmoja ana kundi aliyofungana nalo. Zipo biashara kadhaa za haramu kama pombe, wapo ambao hujiita waislamu wenye kumiliki vilabu au maduka ya bidhaa hiyo, wanahisi mashaka kwani pato kwa upande mmoja limesita na wateja wenyewe ndio hao hao wanaojinasibu na Uislamu kama wao, basi mwezi kama huu kwao ni dhiki tupu, hapa inafaa ieleweke kuwa ikhlasi katika saumu ndio tarajio asisikitike mtu kwa kusita pato hilo ambalo pekee ni haramu tupu. Ni mwezi wakuomba tawba na kumtaka Mola akusamehe kwa kuwanywesha mamia ya waumini kile ambacho Mola alikiharamisha. Mafungu ya madhambi umejitwika nayo wewe ukiwa ni sababu. Ndio maana jiulize “nnafunga kwa kuwa jamii ya kiislamu isinione muovu kwa muda huu tu, lakini muogope Mola ambae anajua ucha mungu wako kwa kutaka kujitakasa khasa au unakoromea moyoni lini mwezi huu wishe niendelee kuangusha makreti”, basi ukiwa upo huko, ipime mwenyewe saumu yako kama mfungaji ina dalili ya kukubaliwa kama unajisemea “aah.. mimi nna malengo yangu” basi sisi wengine hatujui Mola ndiye anayekufahamu kama unamuogopa au humuogopi ni wewe nay eye. Bila shaka wiki iliyomalizia Mwezi wa shaaban nayo iilitwa wiki ya vunja jungu, vunja jungu hili pengine wazee wetu walilengea kufunga mapishi nyakati za mchana au vinginevyo, lakini baadhi tukawa na maana isiyo stahiki, tulidhani tunamkomoa Mola kumbe tukizikomoa nafsi zetu, tulitenda maasi mengi na kufurutu ada, hivyo ndivyo mwezi huu mtukufu unavyokaribishwa na baadhi yetu. Hujisahau tukadhani tutawahi tu Ramadhani kufuta yote yale ambayo tuliyafanya kwa makusudi na kwa akili zetu, yaani kwa wenye kuiona dhiki basi tutende kwa mda ili yale yote maovu na huo mwezi wa kifungo cha mambo yetu aah haya tena hatuna budi, utakwisha na mchezo utapigwa tena mwezi mosi shaawal, yote Mola anayajua kwenye vifua vyetu. Kipindi hiki cha Ramadhani ni muhimu sana kwetu na sio cha kufanyia mzaha. Tumeogelea kwa miezi 11 sasa imepita, tunahitajiwa tusome Qur’aan kwa wingi, tutafute rizki ya halali, tuseme yaliyo mazuri na tuhudhurie mikusanyiko ya kheri kama darsa, nyiradi na dua. Kipindi hiki ndiyo bilisi wa keram,karata,Dhumna na mechi za mpira za Ramadhan ndio huanzishwa eti kupass time, hivi miezi 11 iliyopita haijatosha ? huu mwezi mmoja ndio wa keram na bao na ligi za ulaya hata vipindi vya sala vitupite au tusali bila umakini ili turudi kwenye starehe tusizoweza kuzisamehe!. Itakuwa ni khasara kwetu kama tutapasstime kwa matamanio na michezo. Hatujui nani atakayechukuliwa zamu yake kuelekea kaburini au alieikosa nafasi yakutubia na saa ya kabuli kwake kaipoteza. Tunawasihi na kujinasihi sote tuache yote ya kustarehe tuelekee nyumba za ibada kama hatuna nafasi hiyo basi tukae na familia zetu tusome Qur’aan au kuelekezana mema na kukatazana maovu. MWISHO