Drawer trigger

Saumu Ni Amri Ya Mungu

Sisi kama Waislamu, hatufuati amri yeyote ile ila sharti iwe imenasiwa katika Qur'ani ama katika Hadithi tukufu za Mtume wetu (s.a.w.)

Saumu katika Qur'ani imetajwa kutoka Aya ya 183 ya Sura ya pili 'Albaqarah' hadi Aya ya 187 ya Sura hiyo hiyo. Na Mwenyezi Mungu ametufunza kama ifuatavyo: "Enyi mlioamini, mmelazimishwa kufunga Saumu kama walivyolazimishwa wa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu." "Ni siku chache tu (zinazohesabiwa) lakini miongoni mwenu awaye mgonjwa au katika safari, basi atimize hesabu katika siku zingine. Na wale wanaoweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake basi ni bora kwake, na mkifunga ni bora kwenu mkiwa mnajua." "(Mwezi mnaoambiwa kufunga) ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa mwongozo kwa watu na ishara zilizo wazi za mwongozo na kipambanuzi. “Basi miongoni mwenu atakayeuona mwezi (au atakayekuwa mkazi asiwe msafiri pindi mwezi ufikapo) afunge Saumu na mwenye kuwa mgonjwa au safarini basi atimize hesabu katika siku zingine. Mwenyezi Mungu Huwatakieni mepesi wala Hawatakieni yaliyo mazito, na kamilisheni hesabu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwaongozeni na ili mpate kumshukuru." "Na waja wangu watakapokuuliza juu yangu basi hakika Mimi nipo karibu, Nayaitika maombi ya mwombaji anaponiomba, basi waniitikie na waniamini ili wapate kuongoka." "Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuwaingilia wake zenu (yaani kutangamana nao) wao ni nguo kwenu na nyinyi ni (kama) nguo kwao, Mwenyezi Mungu amejuwa kuwa mlikuwa mkizihini nafsi zenu, kwa hivyo amewakubalieni toba zenu na amewasameheni, basi sasa changanyikeni nao (yaani laleni nao) na takeni aliyowaandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni, mnyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe katika uzi mweusi wa Alfajiri, kisha timizeni Saumu mpaka usiku, wala msitangamane nao na hali mnakaa itikafu misikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu basi msiikaribie. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyobainisha hoja zake kwa watu ili wapate kumcha." Maneno hayo ufasaha usioweza kukabiliwa na mfasaha yeyote, ndiyo asili na misingi ya Saumu. Yeyote abishanaye au kukaidi Amri tunamjibu na kumlainisha kwa nasaha hiyo.