Usiku Mtukufu Wa Laylatul Qadri
Usiku Mtukufu Wa Laylatul Qadri
0 Vote
176 View
"Hakika Tumeiteremsha (Qur'ani) katika usiku wa Laylatul Qadri (Usiku wenye heshima kubwa - ambao nia katika mwezi wa Ramadhani)
Ni nini kitakujulisha usiku huo wa Laylatul Qadri?
Usiku huo (mmoja tu) wa Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu. (97:1-3).
Usiku huu wa Laylatul Qadri kama Mwenyezi Mungu Alivyotudokezea, ni usiku ambao Ameupa heshima kubwa sana hadi ukafikia kuipita miezi elfu (miaka 83 na miezi 4) na hivyo basi anayefanya mema katika usiku huu mmoja tu, huwa sawa na aliyefanya mema kwa muda wa miezi 1000, na afanyaye maovu usiku huu, pia naye huwa amejidhulumu nafsi yake kwa kujichumia adhabu kubwa.
"Inawezekanaje usiku mmoja tu kuishinda miezi elfu?" Hili ni swali wanalojiuliza baadhi ya watu.
Jibu ni: Sote tunaamini ukweli wa Mwenyezi Mungu. Hangeweza kutujuza habari zisizo na ukweli. Pia kulingana na fahamu zetu, hatungeweza kufikia ujuzi wa hali ya juu kama huu. Kwa mfano ambao ni karibu zaidi wa kulifafanua swali hili ni: Lau mtu atapanda mbegu moja ya papai, ambayo kwa kawaida huwa ndogo sana, utastaajabu kuona imetoa tunda ambalo ni kubwa kinyume na mbegu ya embe ambayo ni kubwa na wakati wa kuzaa hutoa tunda dogo, kwa hivyo ni ajabu usiku mmoja tu kuishinda miezi elfu kwa thawabu na utukufu.
Ingawa habari zimewafikiana za kuwako kwa usiku huu mwezi wa Ramadhani, pana hitilafu kubwa sana juu ya usiku wenyewe ni upi? Na huwa tarehe ngapi ya mwezi huu wa Ramadhani? Riwaya kuhusu hoja hii zimefikia 27, na Mwenyezi Mungu mwenyewe Ameificha siku hii makusudi na kutoibainisha ili watu wapate kufanya ibada kwa wingi sana kwakutegemea siku hii kuwa yoyote ile katika mwezi huu kwani lau wangeijua tu basi hata hawangeshughulika katika zile siku zingine.
Ingawa riwaya za usiku huu zimefikia 27, na ingawa usiku huu hasa haujulikani ni upi katika mwezi huu, sisi hufanya A’amaal maalum na mahasusi za usiku huu katika masiku ya 19, 21 na 23.
Masiku haya matatu ya A’amaal ambazo hufanywa, ni Sunna kwa mtu kuoga wakati wa Magharibi.
Pili, wakati huo wa kuanza Ibada husali rakaa mbili ambazo husomwa Surat Alfatiha na Ikhlas mara saba (7) kwa kila rakaa.
Baada ya Sala hii husoma: Astaghfirullaha Rabbi wa atubu ilayhi yaani: "Naomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na ninatubu kwake", mara 70.
Kisha huweka Musahafu mbele yako na kusoma:
Allahuma inni as’aluka bikitabikal munzal. Wa maa fihi wa fihi Ismukal Akbar wa Asmaaukal Husna, wa maa yukhafu wa yurjaa an taj'alani min 'utaqaaika minan-naar.
Yaani: "Ee Mwenyezi Mungu! Ninakuomba kwa utukufu wa kitabu chako hiki - Ulichokiteremsha, na yaliyomo mkiwemo Jina lako kuu na pia Majina Yako Matukufu na Yanayoogopewa na kutarajiwa, Unijaalie niwe miongoni mwa watakoachiliwa na moto".
Kisha omba utakacho.
Baada ya Amali hii utasoma Tawassul hii, na huku umeiwekelea Qur'ani juu ya kichwa:
Allahuma bihaqqe hadhal Qur'ani, wa bihaqqe man arsaltahu bihi, wa bihaqqe kulli mu'minin madahtahu fihi, wa bihaqqiqa alayhim, falaa ahada 'aarafu bihaqqiqa minka.
Hapo endelea na haya mara kumi kumi (10):
Bika ya Allahu; Bi Muhammadin; Bi 'Aliyyin; Bi Fatimah; Bil Hasani; Bil Husayni;
Bi 'Aliy ibnil-Husayni; Bi Muhammad ibni 'Aliyyin; Bi Ja'far ibni Muhammadin;
Bi Musa ibni Ja'farin; Bi 'Aliy ibni Musa; Bi Muhammad ibni 'Aliyyin;
Bi 'Aliy ibni Muhammadin; Bil Hasan ibni 'Aliyyin; Bil Hujjati.
Na sasa omba utakacho.
Sunna nyengine katika masiku haya ni kukesha katika kufanya ibada (si katika kucheza karata) kwani ibada hii ya kukesha ni miongoni mwa yanayomfutia mtu madhambi yake.
Na zaidi ya hayo, kuna sala nyengine ambayo husaliwa rakaa 100 na kila rakaa husomwa Suratul Fatiha na Ikhlasi 10, hivyo basi kuifanya idadi ya Ikhlasi katika sala hii kufikia 1000.
Katika masiku haya Ibada iliyo nzuri zaidi, ni kule kuomba Maghfira (Msamaha) na kuomba haja mbali mbali za hapa Duniani na za Akhera, zako wewe mwenyewe, wazee wako, jamaa, ndugu, majirani na kadhalika Waislamu wote kwa jumla uwaombee.
Vile vile ni Sunna kuyasoma haya mara 100. "Ninakuomba msamaha Mola wangu na ninatubia kwako."
Ama katika usiku wa mwisho, yaani usiku wa kuamkia 23, huzidisha zaidi Ibada ambazo ndizo kinga kwa mwanadamu. Miongoni mwa ibada za usiku huu ni kusoma Suratul Ankabuut, Suratur-Ruum, na Suratud-Dukhaan. Na husoma Dua alizokuwa akizisoma Imam As-Sajjad Zainul Aabidiina Ali bin Hussein (a.s.).
Dua zenyewe huitwa Makaarimul Akhlaaq, na Du’at-Tauba: na kwa kuwa hatungeweza kuziandika zote, tumekifia kwa hizi fupi tu ili atakayetaka zaidi, anaweza kuja kwetu akanunua vitabu vilivyo mahasusi kwa dua za mwezi wa Ramadhani viitwavyo Najaatus-Swaaimiina na Tuh'fatus-Swaaimiina.
Makaarimul Akhlaq:
Ee Mwenyezi Mungu: Mteremshie rehema na amani (mjumbe wako) Muhammad na Aali zake, na imani yangu Uifikishe kwenye ukamilifu wa imani, yakini yangu Uijaalie iwe bora ya yakini, Uifikishe nia yangu hadi kwenye daraja na ubora wa nia, na amali zangu ziwe ni amali bora.
Ee Mwenyezi Mungu, Imakinishe nia yangu kwa upole wako, Uirekebishe yakini yangu kwa ujuzi wako, na Unisuluhishie kwa uwezo wako yaliyoharibika kutokana na mimi.
Du’aut-Tauba:
Ee Mwenyezi Mungu! Kwa hakika mimi ninatubia kwako nikiwa nimesimama hapa madhambi yangu yote makubwa na madogo, vile vile maovu yangu ya ndani na ya dhahiri, pia matelezo yangu yote ya hapo zamani na yatakayozuka.
Ninatubu kwako toba ya yule ambaye hataizushia nafsi yake maasi tena, na asidhamirie kuyarudia makosa kabisa kabisa.