Drawer trigger

Dua Za Kila Siku

Dua hizi zifuatazo husomwa dua moja moja toka mwanzo ya tarehe mosi Ramadhani hadi Muwadda ya mwezi yaani tarehe 30 za Ramadhani.

Kila dua ina siku yake, na inaweza kusomwa mara nyingi kadiri ya uwezo wa mtu mwenyewe. Dua zenyewe ni hizi zifwatazo. 1. Ee Mwenyezi Mungu! Kujaalie kufunga kwangu katika mwezi huu kuwe ni kufunga kwa wanaofunga (Saumu zao zikawa sahihi na kukubaliwa. Na kusimama kwangu kwa ibada kuwe sawa na wanaofanya ibada (zao zikapokelewa), na Uniepushe na usingizi wa wavivu, niwezeshe niukamilishe Ewe Mola wa Walimwengu, na Uniafu Ewe Mwenye kuwasamehe wakosaji. 2. Ewe Mola wangu! Nikurubishe katika mwezi huu karibu na radhi yako, na uniepushe katika mwezi huu hasira zako na maangamizo yako, na Uniwafikie niweze kukisoma kitabu chako Qur'ani Ewe Mrehemevu mno. 3. Ee Mwenyezi Mungu! Niruzuku katika mwezi huu uekevu na uzinduko, Uniepushe Ubaradhuli na upumbavu, na Unijaalie kupata fungu la kila heri itakayoshuka katika mwezi huu ewe Mbora wa wanaokarimu. 4. Ee Mwenyezi Mungu! Nipe nguvu za kuniwezesha kufuata amri zako, Unionjeshe katika mwezi huu Utamu ya kukutaja (kila wakati), Uniwezeshe kutekeleza wajibu wa kukushukuru neema zako na Unihafidhi katika mwezi huu katika ulinzi wako wa sitara yako Ewe Mwenye kuona zaidi ya waoni. 5. Ee Mwenyezi Mungu! Nijaalie katika mwezi huu niwe miongoni mwa wanaoomba maghfira (kwa wingi), pia nijaalie niwe miongoni mwa waja wako wema walio wanyenyekevu, Unijaalie niwe miongoni mwa watu wako walio karibu nawe kwa huruma yako Ewe Mhurumivu wa wanaohurumia. 6. Ee Mwenyezi Mungu! Usinidhalilishe katika mwezi huu kama kilipizo cha kukuasi kwangu, na wala Usinipige katika mwezi huu kwa mjeledi wa maangamizo yako na Uniepushie mbali na mambo yote yawezayo kunitumbukiza katika hasira zako, (nakuomba Unitakabalie maombi yangu haya) kwa Ukarimu wako na Baraka zako Ewe Mwombwa. 7. Ee Mwenyezi Mungu! Niwezeshe na Unipe Nguvu za kufunga (mwezi huu wa Ramadhani wote) na kusimama kwa ibada (zinginezo kama sala n.k.) na Uniepushe na matelezo mbali mbali na madhambi katika mwezi huu, Unidumishe na kukutaja kwa uongozi wako Ewe Mwongozaji wa waliopotea. 8. Ee Mwenyezi Mungu! Niruzuku katika mwezi huu (ili niweze) kuwasaidia mayatima, niwalishe vyakula, pia nijaalie niweze kuwasalimia (Waislamu wote) kila nikutanapo nao, Unijaalie kuhusubiana na watukufu (uwapendao) kwa utajiri wako Ewe Makimbilio wa wahitaji. 9. Ee Mola wangu! nijaalie katika mwezi huu nilipate fungu la rehema zako pana, Uniongoze katika mwezi huu kwenye mwanga wako unaong'ara, na Uniongoze moja kwa moja kwenye radhi yako yenye kukusanya mahaba yako (yaani mambo yote Unayoyapenda na kuyaridhia) Ewe Karim. 10. Ee Mwenyezi Mungu! Nijaalie katika mwezi huu niwe mwenye kukutegemea, pia Unijaalie miongoni mwa watakaofuzu kwako, pia nijaalie katika mwezi huu niwe miongoni mwa watakaokurubishwa kwako kwa Wema wako Ewe mpaji wa wanaoomba. 11. Ee Mwenyezi Mungu! Nijaalie nipende sana kutenda mema katika mwezi huu, na Unichukizishe katika mwezi huu kutenda maovu na uasi. Unikingie katika mwezi huu hasira zako na moto kutokana na msaada wako Ewe Mnusuru wa wanaotaka kunusuriwa. 12. Ee Mwenyezi Mungu! Nipambe katika mwezi huu wa Ramadhani kwa sitara yaani (vazi) la kukuogopa, na Unisitiri katika mwezi huu kwa vazi la kukinai na kutosheka, na Unielekeze katika mwezi huu kwenye uadilifu na usawa. Na Unisalimishe katika mwezi huu na kila nikiogopacho kwa kinga yako Ewe Mhifadhi wa wenye kuogopa. 13. Ee Mwenyezi Mungu! Nitakase nitokamane na taka na uchafu (mwengine), Unipe subira (ili nisubiri) katika mwezi huu juu ya matukio ya Kudira zako, Uniwafikie kwenye kukucha (kukuogopa) na kusuhubiana na wema, kwa msaada wako Ewe Kiburudisho (kitulizo) cha macho ya walio maskini. 14. Ee Mwenyezi Mungu! Usinihukumu/kunilaumu kwa makosa, katika mwezi huu, Uniepushe na kunipunguzisha na makosa na matelezo, na wala Usinifanye lengo la balaa na maafa katika mwezi huu, Kwa Utukufu wako Ewe Utukufu wa Waislamu. 15. Ee Mwenyezi Mungu! Niruzuku utiifu wa wenye kunyenyekea katika mwezi huu, na Unikunjue kifua changu katika mwezi huu kwa toba za wenye kunyenyekea kwa Amani yako ewe Amani ya wenye kuogopa. 16. Ee Mwenyezi Mungu! Niwafikie katika mwezi huu kwa kusikizana na watu wema, na Uniepushe katika mwezi huu kurafikiana na wabaya, Uniweke kwa Rehema yako kwenye Nyumba ya Utulivu kwa Utukufu wako Ee Bwana Mwabudiwa wa viumbe. 17. Ee Mwenyezi Mungu! Niongoze katika mwezi huu kwenye amali njema, Unitekelezee katika mwezi huu haja zangu na mataraji yangu, Ewe Usiyehitaji ufasiri na kuuliza (ndipo ukaifahamu haja ya mja, bali Unaifahamu hata bila ya kuuliza na bila kuelezwa). Ewe Mjuzi wa yalioyomo vifuani (nyoyoni) mwa walimwengu! Mteremshie rehema na amani (Mtume) Mohammad (s.a.w.) na Aali zake watakatifu. 18. Ee Mwenyezi Mungu! Nizindushe katika mwezi huu ili nipate baraka za masiku yake, Uninawirishe moyo wangu kwa mwangaza wa nuru zake (Nuru za mwezi huu wa Ramadhani) Uvishike viungo vyangu vyote viwe ni vyenye kufuata nyayo zake, kwa Nuru yako ewe Mwangaza wa nyoyo za wakujuao. 19. Ee Mwenyezi Mungu! Niongezee fungu langu la baraka za mwezi huu, na Unisahilishie njia ya kuyafikia mema ya mwezi huu, wala Usininyime kukubaliwa mema, Ewe Aongozaye kwenye haki iliyo wazi. 20. Ee Mwenyezi Mungu! Nifungulie milango ya peponi (ili niingie kwa haraka), na Unifungie milango ya moto (ili nisipate kuingia humo) Uniwafikie kuisoma Qur'ani kwa wingi sana katika mwezi huu, Ee Mwenye kutia utulivu nyoyoni mwa wenye kuamini. 21. Ee Mwenyezi Mungu! Nioneshe njia ya kuifikia Radhi yako, wala Usimpe Shetani nafasi ya kunihangaisha katika mwezi huu. Uijaalie Pepo iwe ndiyo mashukio yangu na mapumziko. Ewe Mwenye kuzitekeleza haja za wakuombao. 22. Ee Mwenyezi Mungu! Nifungulie katika mwezi huu milango ya fadhila zako, na Uniteremshie katika mwezi huu baraka zako Uniwafikie katika mwezi huu niyatende yanifikishayo kwenye Radhi yako, Uniweke katika pepo yako uipendayo ewe Mwitika wa maombi ya wenye dhiki. 23. Ee Mwenyezi Mungu! Nisafishe katika mwezi huu ili nitokamane na madhambi, Unitakase na aibu (zote) Uuonjeshe moyo wangu Taqwa ya nyoyo (za wanaokuogopa) Ewe Msamehevu wa matelezo ya wenye dhambi. 24. Ee Mwenyezi Mungu! Ninakuomba katika mwezi huu (Unijaalie niyatende) yanayokuridhisha. Na ninajilinda kwako na yanayokuudhi. Na ninakuomba kuniwafikia katika mwezi huu nikutii pasina kukuasi, Ee mpaji wa wakuombao. 25. Ee Mwenyezi Mungu! Nijaalie katika mwezi huu niwe mwenye kuwapenda watu wako (uwapendao) na unijaalie niwe mwenye kutenda Sunna za Mtume wako wa mwisho (Muhammad (s.a.w.)). Ewe Mwenye kuzitakasa nyoyo za Mitume. 26. Ee Mwenyezi Mungu! Ujaalie mwendo wangu (yaani juhudi zangu na bidii) uwe ni wenye kushukuriwa, yaani kulipwa mema, na dhambi zangu ziwe zenye kusamehewa, amali zangu ziwe zenye kusitiriwa, Ee Msikiaji zaidi wa wanaosikia. 27. Ee Mwenyezi Mungu! Niruzuku katika mwezi huu fadhila za usiku wa Laylatul Qadri, Uyageuze mambo yangu yaliyo mazito ili yawe mepesi. Uzikubali nyudhuru zangu, Uniepushe (na Unifutie) madhambi na makosa (mengine) Ee mpole kwa waja wema. 28. Ee Mwenyezi Mungu! Niongezee fungu langu la mwezi huu kutokamana na nyongeza, unikirimu katika mwezi huu niyakinishe maombi. Njia zangu za kukufikia ziwe karibu miongoni mwa njia. Ee Usiyeshughulishwa na mahimizo ya wahimizao. 29. Ee Mwenyezi Mungu! Nifunike katika mwezi huu kwa rehema, Uniruzuku uongofu na kulinda na machafu, Utahirishe moyo wangu usiingiwe na giza la shaka Ewe Mrehemevu wa waja wako walio wema. 30. Ee Mwenyezi Mungu! Ijaalie Saumu yangu niliyoifunga mwezi huu wote iwe ni sahihi yenye kukubaliwa (iwe yenye kufungamana) na Uyaridhiayo na ayaridhiayo Mtume (s.a.w.) (Ijaalie Saumu yangu) iwe madhubuti ya shina na matawi kwa haqqi ya Bwana wetu Muhammad (s.a.w.) na kizazi chake walio watakatifu Wal Hamdu Lilahi Rabbil Aalamiin.