'Nafsi' Ni Adui
'Nafsi' Ni Adui
0 Vote
148 View
Mwenyezi Mungu Anasema, "Na kiwe katika nyinyi (Waislamu) kipote ambacho kitawalingania watu katika mambo ya kheri, kiwe kinaamrisha mema na kinakataza maovu.”
Kuamrishana mema na kukatazana maovu ni jambo la lazima kwa kila mwislamu awaye mume au mke, na hasa wakati wa Ramadhani.
Ingawa mwezi huu mashetani hufungwa kama ilivyopokewa katika hadithi, pana adui mwengine kwa mwanadamu ambaye husononeka sana anapomwona mwanadamu katika mwangaza wa utiifu, na ye si mwengine bali ni "Nafsi". Mungu Asema: "Nafsi ni yenye kuamrisha (sana) maovu."
Mmoja wa wanavyuoni asema: "Nafsi ni kitu kiovu zaidi ya mashetani elfu."
Nafsi hii hii ndiyo ambayo huwaghafilisha baadhi ya watu wasifunge mwezi huu, wala wasikumbuke kabisa adhabu ziwasubirizo wasiofunga.
Mtume (s.a.w.) alisema "Watu wasiofunga hufungwa miguu yao kwa pingu kisha wakaninginizwa vichwa vyao chini na miguu yao juu na huku wapigwa na kucharazwa mijeledi kemkem, pia huwa nyuma yao wale wanaokula kabla ya wakati maalum wa kufuturu haujafika."
Jee ndugu waona!!! Lakini lao kubwa ni kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani: "Hakika wao wanaoiona (siku ya kiama) iko mbali nasi Tunaiona iko karibu sana."
Pia wanaofunga na huku hawasali, wao ni mfano mbaya sana kwa umma wa Kiislamu. Allah Anasema, "Adhabu kali sana itawathibitikia wale wanaosali na ambao wao katika sala zao hughafilika."
Waliokusudia hapa ni watu ambao wao husali leo kesho hawasali, husali asubuhi jioni hawasali na kadhalika. Ikiwa Mwenyezi Mungu Amekasirika hivyo hadi kufikia hatua ya kuapa kuwatia adabu wasiosali sawasawa, waonaje kwa yule asiyesali kabisa? Ama wasiosali wamewekeana mkataba na Mwenyezi Mungu wa kusameheana?