Drawer trigger

Uislamu Chaguo Langu 19 + Sauti

Sikiliza Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki kinachowaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina wameamua kufuata njia ya haki na ukamilifu maishani ambayo ni njia ya Uislamu. Leo tutamuangazia Mmarkani aliyesilimu, Bi. Aminah Zahira. @@@ Yeye ni mzaliwa wa mji wa Tucson katika jimbo la Arizona nchini Marekani, Ni ni mwanamke mkarimu na malenga mwenye kipaji. Binafsi anasema hivi: "Mimi ni mwanamke Mwislamu mbunifu, nina malengo ya juu na nataka kuelekea peponi. Nimezaliwa upya na sasa kama mbegu iliyopandwa nasubiri fursa bora zaidi kuchipua ili niweze kueneze manukato yangu bora kote duniani. 'Mwenye kusema maneno haya ni Bi. Brandy Chase ambaye baada ya kusilimu alichagua jina la Aminah Zahira na sasa yeye ni Mmarekani Mwislamu.' Kwa mtazamo wa Wamagharibi waliowengi, wanawake Waislamu  wamedhulumiwa sana na haki zao zinakiukwa na wanaume. Lakini pamoja na kuwepo propaganda zote hizo chafu za Wamagharibi kuhusu hali la wanawake katika Uislamu, tunashuhudia kuongezeka idadi ya wanawake Wamagharibi wanaosilimu.  Wanawake wamagharibi waliosilimu, kwa kuukubali Uislamu wanahisi kuwa si tu kuwa hawana vizingiti bali Hijabu inawapa uwezo wa kujisitiri na hivyo kuwa mbali na ufisadi wa kimaadili katika jamii za Kimagharibi. Wanawake Waislamu wana nafasi muhimu katika familia na jamii na kwa harakati zao katika fremu ya Uislamu wameweza kuondoa taswira potofu kuhusu mwanamke Mwislamu. Amina Zahira ambaye ni mwandishi , malenga , mchoraji na mwandishi blogu anafafanua hizi kuhusu namna alivyosilimu.: 'Mimi nilizaliwa Mkristo na niliendelea kuwa Mkristo hadi nilipokuwa na umri wa miaka 14. Hapo niliachana na Ukristo kwa sababu ulikuwa haukidhi mahitaji yangu nikaendelea na maisha kama mulhidi au kafiri.  Sikuwa namuamini Mungu. Lakini baada ya muda usio mrefu nikaamua kufanya utafiti kuhusu dini ya kufuata maishani. Alhamdulillah Mwenyezi Mungu aliniongoza katika Uislamu nikiwa bado kijana." Amina Zahira aliweza kupata maarifa kuhusu umaridadi wa Uislamu na mabadiliko haya ya kina katika maisha yake yanahisika katika hadithi anazoandika. Hivi sasa anatumia kipawa chake cha uandishi kuhudimia Uislamu. Anasema hivi kuhusu taalaum yake ya uandishi: 'Baada ya kusilimu nilibadilisha kwa kiasi kikubwa mtindo wangu wa uandishi. Kisha nilianza kuchora katuni kuhusu matatizo katika Jamii ya Marekani. Kabla ya kusilimu nilikuwa nimezoea kuandika mashairi kuhusu maisha na chuki yangu kuhusu dini. Sasa si hivyo tena!. Hivi sasa nafurahi kuandika kumhusu Allah SWT ili kuwaonyesha wengine ukarimu na utulivu ulio katika Uislamu.' Anaongeza kuwa: "Watu wengi wasiokuwa Waislamu Marekani na kote duniani wamesema kazi zangu. Wanasema vitabu vyangu vimewapa ilhamu na kuwawezesha kuujua Uislamu na kugundua mengi mapya kuhusu dini hii tukufu. Jamaa zangu si Waislamu lakini baada ya kusoma hadithi na mashairi yangu wameweza kufaidika ingawa si Waislamu.' Kawa mtazamo wa Uislamu suala la kuwahudumia viumbe ni mwanzo wa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na pia katika upande mwingine kadiri mtu anavyopata maarifa kuhusu Mwenyezi Mungu anajawa mapenzi katika kuwahudumia wanaadami. Kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume SAW, kuwahudumia watu ni jambo linaloenda sambamba na kumuamini Mwenyezi Mungu. Mtume SAW anasema: "Kumuamini Mwenyezi Mungu na kuwanufaisha waja wake ni sifa mbili nzuri na hakuna lililo juu ya hayo mawili". Bi. Zahira kwa imani yake kuhusu akhera na kudiriki lengo na uhakika wa maisha anasema kuwahudumia wengine na kuwasaidia Waislamu ni msingi muhimu katika maisha. Anaendelea kusema: 'Hatimaye katika siku ya qiyama tutaulizwa kuhusu maisha yetu. Yamkini mipaka ya nchi ikabadilika, lakini Uislamu na misingi yake itabakia daima. Katika Uislamu tunawajibu wa kuwasaidia kwanza ndugu zetu Waislamu na baada ya hapo tuwasaidie wengine wanaohitaji. Kwa hivyo naamini kuwa tunapaswa kudumisha umoja wetu.' @@@ Bi. Amina Zahira mwanamke huyu Mmarekani aliyesilimu anasema pamoja na kuwepo mashinikizo yote katika maisha yake, ameuchaguai Uislamu na atajitahidi kueneza dini hii tukufu miongoni mwa Wamareknai. Bi. Zahira anasema hivi kuhusu juhudi zake na za Wamarekani Waislamu wenzake katika kuwasilisha taswira sahihi ya Uislamu na umaridadi wake kwa wengine. Anasema hivi: 'Waislamu wa Marekani kimsingi ni watu wakarimu na aghalabu ni wasema kweli na watenda amali njema. Wanataka kueneza Uislamu wa kweli na wakati mwingi wasio kuwa Waislamu huvutiwa na amali za Waislamu.' Haki za wanawake katika Uislamu zinawabainikia kwa njia bora zaidi wanawake ambao wamesilimu kwani tayari huwa wanajua kikamilifu mitazamo ya itikadi zingine kuhusu wanawake. Bi. Zahira vile vile anahisi tafauti hizi na ndio jambo lililompelekea asilimu na hivyo kuukubali mtazamo wa Uislamu kuhusu mwanamke. Anaendelea kusema hivi: "Wanawake waliosilimu wanajitahidi kuwa na tabia njema  zinazoenda sambamba na vazi la Hijabu wanalovaa . Kwa njia hiyo wanadhihirisha pia mahaba yao kwa dini tukufu ya Kiislamu. Katika miji mingi ya Marekani watu wanajua tu yale wanayosikia katika vyombo vya habari. Kwa mfano iwapo kutaenea habari kuwa huko Saudi Arabia mwanamke aliye gerezani amezuiwa kumuona mtoto wake wote hufikiri kuwa serikali za Mashariki ya Kati ni hatari na ni tishio kwa usalama wa dunia. Lakini ukweli ni kinyume na hilo kwa Uislamu unapinga sera zote zinazomdhalilisha mwanamke na badala yake unawaongeza wanawake katika njia ya izza ya nafsi na kujiamini.' Wapenzi wasikilizaji katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia kuimarika harakati ya kuutaka na kuuhitajia Uislamu katika nchi za Magharibi. Kwa hakika, kwa karne kadhaa sasa jamii ya magharibi  imekuwa ikikumbwa na ina kiu kali ya haki na umaanawi. Hitajio hili liko miongoni mwa watu binafsi na pia katika umma. Katika nchi za Magharibi tunashuhudia pengo kubwa la umaanawi katika maeneo ya ummah kama vile sehemu za kazi, shule, vyuo vikuu, masoko, serikalini, katika vyombo vya habari n.k. Tatizo la ukosefu wa umaanawi linashuhudiwa pia katika familia ambayo ni msingi wa jamii. Mgogoro mkubwa wa utambulisho sawia na hitajio shadidi la umaanawi ni mambo ambayo yamepelekea Wamagharibi kuelekea katika dini kama  vile Ubuda na Uhindu. Lakini kutokana na kuwa dini kama hizo hazina uwezo wa kukidhi mahitajio ya mtu binafsi na jamii, wengi sasa wanaelekea katika Uislamu. Wamagharibi wengi wametambua ukweli huu kuwa katika Uislamu, umaanawi na maadili bora yako katika kila uga wa maisha ya mtu binafsi na jamii. Kimsingi wametambua kuwa Uislamu ni mfumo kamili wa maisha na kwa kufuata dini hii tukufu wanaweza kupata tena umaanawi na muelekeo katika maisha ya dunia na akhera. http://kiswahili.irib.ir