Zaka Ya Fitri
Zaka Ya Fitri
0 Vote
112 View
"Hakika amekwisha faulu aliyejitakasa (na mabaya kwa kutoa zaka) na akakumbuka jina la Mola wake na akasali." 87: 14-15.
Zaka ya Fitri ambayo kwa jina jengine huitwa 'Zaka ya kiwiliwili' ni faradhi ambayo ilifaradhiwa ili kuwatakasia waliofunga Saumu zao.
Zaka hii ya Fitri, humlazimu mtu aliyebaleghe, aliye na akili, huru, na mwenye kuweza.
Mbali na kuwa utakaso kwa viwiliwili, Fitri hii huwa ndicho kifurahisho kwa asiye na uwezo ili naye apate kufurahia siku ya kufuturu (siku ya Iddi) kama wenzake.
Aliyeyatimiza masharti ya kuitoa zaka hii, hulazimika kujitolea yeye mwenyewe na kumtolea kila anayehesabika kuwa wa familia yake na anayemlazimu kumlisha hata kama ni mgeni akiwa alimjia kabla ya kuingia usiku wa kuamkia Iddi. Ama mgeni aliyefika baada ya kuingia usiku, na mtoto aliyezaliwa baada ya kuingia usiku, yaani Magharibi, hawalazimu kuwatolea zaka hii ya Fitri.
Wakati wa kuitoa, ni baada ya kuingia usiku wa kuamkia Iddi, na ni vizuri zaidi kuitoa kabla ya Kusali sala ya Iddi.
Kitolewacho ni tende, ngano, shayiri (barley) na zabibu au kiwango (senti) cha chakula kitumikacho zaidi nchini. Kila mtu hutolewa pishi (kilo tatu - 3kg).
Wapewao zaka hii ya Fitiri, ni Waislamu wenye imani wasiojiweza. Ni Sunna kuwatanguliza katika ugawanyaji, watu wako, yaani wa ukoo wako, kisha majirani walio fukara (maskini). Na miongoni mwa wanaostahili kupawa, ni vyema kuwatanguliza wenye elimu kisha wenye dini zaidi. Ama (Mwisilamu) mlevi, na asiyesali watu hao hawapawi.