Uislamu Chaguo Langu 18 + Sauti
Uislamu Chaguo Langu 18 + Sauti
0 Vote
271 View
Sikiliza Mwenyezi Mungu SWT ndio mhimuli wa uongofu na amali njema. Yeye ni nuru kubwa ambayo huwaangazia wanaadamu na kuwapa saada. Mwanaadamu naye pia ameumbwa ili aweze kuyafikia malengo ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo tunaweza kusema muongozo au hidaya ni jambo la kimaumbile. Lakini baadhi ya masuala ya kimaisha na upotofu katika mazingira ya jamii hupelekea mwanaadamu kuondoka katika mkondo sahihi wa maisha. Pamoja na hayo mwanaadamu katika kufuata dhati ya maumbile yake hujitahidi kutafuta ukweli ili hatimaye aweze kufaidika na nuru ya Mwenyezi Mungu. Hii ni nuru ambayo sasa iko katika nyoyo za waumini wa kweli na wenye ikhlasi. Mwenyezi Mungu SWT katika aya ya 35 ya Suratun Nur anasema hivi: "Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. Katika upeo wa nuru ya Mwenyezi Mungu, nyoyo ziko tayari kupokea ukweli na muongozo maishani. Wanaadamu wengi wakati wanapoishi maisha ya upotofu; ijapokuwa kidhahiri hawawezi kukiri lakini huwa wanapata masaibu ya kinafsi. Wenye kupata taufiki hatimaye hufikia imani ya Mwenyezi Mungu na kukiri kuwa wameingia katika maisha mapya na hivyo huwa kana kwamba wamezaliwa upya. Wapenzi wasikilizaji karibuni kujiunga nami katika dakika hizi chache za makala yetu hii yenye anuani ya 'Uislamu Chaguo Langu' ili tuweze kuangazia maisha ya Joseph Zammit, raia wa Malta aliyesilimu baada ya kufanya utafiti wa kina. Leo @@@ "Tokea utotoni, kutokana na mapenzi ambayo Mwenyezi Mungu aliyatia katika moyo wangu, nilikuwa navutiwa na masuala ya kimaanawi na kidini. Daima wakati mama yangu alipokuwa akifanya kazi za nyumba, alikuwa akinisimulia visa vya maisha ya Nabii Issa AS. Niliutumia wakati wangu wa mapumzko kusoma visa vya mitume na watu wakubwa waliotangulia na hasa nilivutiwa sana na shakhsia ya Nabii Issa AS. Nilishiriki katika masomo ya kujifunza Bibilia. Hapo niliweza kupata yakini kuwa kuna sehemu kubwa ya maneno ya Injili ambayo yalikuwa yamefutwa. Kwa hivyo singeweza tena kuyakubali mafundisho ya Kikristo kwani hayakuwa yananiathiri tena. Niliacha kila kitu mikononi mwa Mwenyezi Mungu na nikaamua kuanza kufanya utafiti kuhusu dini mbali mbali. Kwa hakika nilikuwa namtafuta Mwenyezi Mungu na nilifanya kila niwezalo ili kumfikia naye pia alinisaidia katika hili." Maneno hayo ni sehemu ya kumbukumbu za Joseph Zammit, raia wa Malta aliyesilimu na kuchagua jina la Yusuf Abdullah. Kuhusu tajriba yake katika kuutafuta ukweli, Yusuf Abdullah anaendelea kusema hivi: 'Kufuatia kuongozeka moyo wa kutafuta ukweli katika nafsi yangu, nilianza kufanya utaifti kuhusu makundi mbali mbali ya Kiirfani pamoja na nadharia mbali mbali za kisaikolojia. Halikadhalika nilifanya utafiti kuhusu dini ya Ubuda. Sambamba na hilo nilichunguza pia itikadi za Kisufi na nikapata nukta za kuvutia lakini kutokana na kuwa chimbuko lake lilikuwa ni Uislamu, sikuendeleza utafiti kuhusu Usufi. Hii ni kwa sababu nilikuwa nimesikia sifa mbaya za Uislamu kama vile dini hii ni ya vita na inayokinzana na uhuru. Nilifanya utafiti kuhusu Irfani ya Kihindu na mapote ya Kikristo. Utafiti huu ulipelekea nichunguze Bibilia kwa kina. Pamoja na hayo nilikuwa navutiwa na Uislamu kutokana na usahali na mapenzi ya kina ya Waislamu kwa Mwenyezi Mungu." Pamoja na kuwepo propaganda chafu dhidi ya Uislamu lakini Yusuf Abdullah alikuwa anahisi kuwepo sauti ya ndani iliyokuwa inamuita kuelekea katika Uislamu. Hatimaye Mwenyezi Mungu aliitikia dua yake na akaweza kuifahamu Qur'ani ambayo ni kitabu kamili zaidi na cha mwisho kutoka kilichoteremka kutoka mbinguni. Yusuf Abdullah anabainisha hivi kuhusu kusilimu kwake: "Katika nchi ya Kikatoliki kama Malta, ambayo ni nchi ndogo kusini mwa bara Ulaya, kuwa Mwislamu kunahesabiwa kuwa ni uhaini mkubwa. Kutokana na hili nilinyanyua mikono yangu juu na kumuomba Mwenyezi Mungu anipe hidaya. Raghba kubwa katika nafsi yangu ilkuwa cheche ambayo ilinipelekea nifanye utafiti wa kina kupitia kuisoma Qura'ani Tukufu. Baada ya kuona mshabaha mkubwa katika yaliyomo ndani ya Qur'ani na Injili kuhusu Mitume waliotangulia. Nilishangaa ni vipi katika miaka yote ya utafiti wangu sikuwa bado nimeisoma Qur'ani." Kwa msingi huo Yusuf Abdullah aliweza kujifunza mengi katika Qur'ani Tukufu na hivyo akafaidika na mafundisho yake yenye kuleta utulivu moyoni. Anaendelea kusema hivi: "Nilianza kusoma Qur'ani kila siku na hatua kwa hatua nikaanza kujifunza kuhusu nguzo za Uislamu kama vile Sala, Saumu, Hija na kadhalika." Kati ya mambo yaliyomvutia sana Yusuf Abdullah kabla ya kusilimu ni umaridadi wa ibada ya Hija. Alikuwa na hamu sana ya kushiriki katika kongamano hili adhimu la Waislamu. Mwenyezi Mungu alitaka aelekee Hija kama Mwislamu kamili. Anaendelea kusema hivi: 'Nikiwa katika msikiti wa eneo langu nilikutana kwa sadfa na mtu na mkewe ambao walikuwa raia wa Uingereza. Tulifanya mazungumzo na wakanizawadia vitabu kadhaa. Vitabu hivyo vilikuwa ni vyenye thamani sana kwani baada ya kuvisoma niliweza kutambua ukweli na kupata yakini kuhusu nuru ya Uislamu na Ushia na hapo nikaamua kuikumbatia kikamilifu dini ya Kiislamu na hivyo baada ya kusilimu na kwa imani imara ya Ushia nilielekea katika safari ya Hija." @@@ Mpenzi msikilizaji kama mjuavyo tunakaribia msimu wa Hija ambao ni machipuo ya umaanawi na dhihirisho la Tauhidi. Wenye kupata taufiki ya kutekeleza ibada ya Hija ipasavyo huibuka wakiwa wametakasika kikamilifu. Katika ibada ya Hija nuru ya utakasifu huweza kuonekana na Waislamu pamoja na wasiokuwa Waislamu. Hii ndio sababu wengi waliosilimu huvutiwa sana na ibada hii kwani mvuto wake hauko katika dini au itikadi yoyote nyingine. Kwa mfano Malcolm X aliyekuwa kiongozi wa Waislamu Marekani alielekea Hija baada ya kusilimu. Anasimulia ifuatavyo safari yake ya Hija. "Hadi sasa sijawahi kuona idadi kubwa ya watu kama hii ambapo wote wanafanya ibada pamoja kwa raghba kubwa na kwa hisia ya udugu. Hapa ni ardhi ya kale na palikuwa makao ya Ibrahim AS na Mohammad SAW pamoja na Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu. Wote, kutoka kila rangi na kaumu wamekutana katika sehemu moja pasina kuwepo ubaguzi. Katika wiki nilizokuwa Hija nilivutiwa sana kwa ajili ya kuwa katika mjumuiko huu na hata sina maneno ya kuelezea hisia niliyokuwa nayo." Hivi sasa baada ya kusilimu, Yusuf Abdullah anamuomba Mwenyezi Mungu aweze kuwaongoza wanaadamu wote katika njia ya haki. Anasema pamoja na kuomba dua, mwenye kutaka hidaya pia anapaswa kuwa na raghba na bidii ya kutafuta ukweli. Yusuf Abdullah, raia wa Malta aliyezaliwa Mkristo na baadaye kusilimu baada ya kufanya utafiti anasema hivi kuhusu kuishi katika nuru ya Uislamu: "Katika kutaka Mwenyezi Mungu atuongoze katika njia ya haki tunapaswa kuwa wakweli na kisha tumuachie mengine yote. Katika maisha yangu ya kabla ya kusilimu nilikuwa navutiwa na vitu vya kidunia. Lakini sasa kuwepo Mwenyezi Mungu katika maisha yangu ni jambo ambalo limepelekea nipate utulivu maishani. http://kiswahili.irib.ir