mikesha_ya_peshwaar
mikesha_ya_peshwaar
(0 Kura)
(0 Kura)
mikesha_ya_peshwaar
Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza kiitwacho, Peshawar Nights. Asili ya kitabu hiki ni cha lugha ya Kifarsi kwa jina la, Shab’ha-ye Peshawar. Sisi tumekiita, Mikesha ya Peshawar. Mikesha ya Peshawar ni nakala ya mjadala kati ya wanavyuoni mbalimbali wa Kisunni na mwanachuoni mmoja wa Kishia mzaliwa wa Shiraz (Iran) aitwaye Sayyid Abdu ‘l-Fani Muhammad al-Musawi Sultanu ‘l-Wa’idhiin, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 31 tu. Mjadala huu ulifanyika katika mji wa Peshawar ambao wakati huo ilikuwa ni sehemu ya Bara Hindi na hivi sasa ni sehemu ya Pakistan. Ulifanyika kuanzia tarehe 27 Januari 1927 na kuundelea kwa mikesha kumi ndani ya msikiti ambako watu zaidi 200 walihudhuria kila usiku. Mjadala huu ulifanywa kwa muundo mzuri wa kuheshimiana pande zote bila ya kuvunjiana heshima. Mwandishi mwenyewe amejiita katika kitabu hiki kama “Da’i” yaani mtu anayewaombea mema watu wengine, sisi tumelitafsiri neno hilo kama “Muombezi”. Masharti ya mjadala yalikuwa kwamba ni vianzo vile tu vinavyokubaliwa na madhehebu zote ndivyo vitakavyorejelewa. Mjadala huu uliandikwa na kuripotiwa na waandishi wanne katika magazeti ya kila siku, na baadaye ukachapishwa kama kitabu huko Tehran, Iran. Huu ulikuwa ni mjadala uliopangwa vizuri, wa kielimu na utumiaji wa vipawa vya akili ambapo kila hoja iliyotolewa ilitumika elimu na akili kuiwasilisha mpaka pande zote zikaridhika. Katika kuwasilisha hoja zake, mwanachuoni huyu mkubwa wa Kishia alitumia rejea za vitabu vingi maarufu vya Kisunni na ambavyo si maarufu sana lakini vyenye kuaminika. Rejea na vitabu hivyo vimeorodheshwa kwa wingi sana ndani ya kitabu hiki ili msomaji aweze kuvirejelea. Lakini kwa bahati mbaya sana, mengi ya matoleo mapya ya vitabu hivyo yamefanyiwa mabadiliko na baadhi ya sehemu kuondolewa, hususan zile zinazounga mkono madai ya Shia. Ufuatao hapa chini ni mfano mdogo tu wa yanayofanywa katika vitabu hivyo: Katika ukurasa wa 301 wa juzuu ya 3 ya Tafsir al-Kashshaaf iliyokusanywa chini ya maelekezo ya Sheikh Mustafa al-Halabi (toleo la pili, 1319 A.H. liliochapishwa na Main Government Printing House ya Amiriah Bulaq ya Misir), kuna beti zinazojitokeza ambazo kwazo Jarullah Zamakhshari, mfasiri wa al- Kashshaaf, alitangaza wazi imani yake katika uhalali wa Ushia. Lakini katika chapisho la 1373 A.H. lililochapishwa na Printing House Istiqamah bi’l-Qahara, shairi lililotajwa halionekani tena. Marehemu Allamah Sayyid S. Akhtar Rizvi katika kitabu chake Uimamu uk. 37, anaandika kushangazwa kwake kutokana na maneno yaliyoondolewa katika kitabu cha at-Tarikh cha at-Tabari, chapa ya Leiden (ya mwaka 1879 Masihia) ambayo imeyanakili maneno ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) aliyoyatumia wakati wa karamu maarufu ya ndugu wa karibu aliyoitayarisha mwenyewe.