Uislamu Chaguo Langu 22
Uislamu Chaguo Langu 22
0 Vote
157 View
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala nyingine ya 'Uislamu Chaguo Langu' ambayo huwaangazia watu ambao, baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kubadilisha mkondo potofu maishani na kufuata njia iliyonyooka na iliyojaa nuru ya Uislamu. Hakuna shaka kuwa kila mwanaadamu mwenye kiu ya kutafuta maana katika maisha yake, hatimaye hufikia lengo analokusudia. Katika makala ya leo tutamuangazia mhubiri maarufu wa kikristo kutoka Canada aliyesilimu Dkt. Garry Miller na Daniel Streich mwanasiasa Mswisi ambaye aligeuka kutoka kuwa Mkristo mwenye chuki dhidi ya Uislamu hadi Mwislamu mwenye kusimamisha sala tano kwa siku. Wote hawa walisilimu baada ya kuutambua ukweli. Karibuni kujiunga nami hadi mwisho. Moja ya mbinu ambazo zinatumiwa na nchi za Magharibi katika kukabiliana na Uislamu ni kuhimiza sera ya chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia. Kwa mujibu wa sera hiyo, Uislamu na Waislamu huarifishwa kama hatari kubwa kwa ulimwengu wa Magharibi. Sera hii pia hutumiwa kuwawekea vizingiti vingi Waislamu waishio katika jamii za nchi za Magharibi. Ili kufikia malengo hayo, mashirika yaliyo dhidi ya Uislamu yameanzishwa Ulaya na Marekani kwa lengo la kuwatia watu hofu kuhusu Waislamu kwa makusudio ya kutoa pigo kwa Uislamu na kwa upande wa pili kuonyesha kuwa eti ustaarabu wa Magharibi ndio ustaraabu bora duniani. Kuenea kwa kasi Uislamu katika jamii za Wamagharibi ni jambo ambalo limepelekea mashirika yaliyo dhidi ya Uislamu kukithirisha propaganda zao potofu dhidi ya dini hii tukufu. Hivi leo mijadala kuhusu Uislamu inafanyika kwa upana katika vyombo vya habari vya kimagharibi. Philip Rondeau mwandishi mwenye misimamo mikali wa Kimagharibi anasema hivi: "Waislamu ni kama bomu na Uislamu unawavutia wengi hasa watu wa Ulaya." Jarida lenye wasomaji wengi la TIME katika makala yenye kuwatusi Waislamu lilitaja kuongezeka idadi ya Waislamu kuwa ni 'Mgogoro wa Utambulisho Ulaya.' Katika toleo hilo la Julai 13 mwaka 2006, picha iliyoandamana na makala hiyo ilikuwa na mchoro maarufu wa karne ya 15 Miladia wenye taswira ya mwanamke ajulikanaye kama Monalissa akiwa amevaa Hijabu ya Kiislamu. Makala hii ilikuwa na lengo la kuonyesha kuenea Uislamu katika kitovu cha utamaduni wa Ulaya na hivyo kuwachochea wasomaji wazuie hali hiyo kuendelea. Katika kuendelea hatua za chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya, mwishoni mwa mwaka 2010 nchini Uswisi tulishuhudia kupigwa marufuku ujenzi wa minara katika misikiti yote ya nchi hiyo. Sheria hiyo ya kustaajabisha ilipitishwa kupitia kura ya maoni kote Uswisi. Pendekezo hilo la kupigwa marufuku minara liliwasilishwa na chama cha Kikristo kijulikanacho kama Chama cha Wananchi (SVP). Chama hicho kilifanya juu chini kuhakikisha kura hiyo ya maoni inafanyika kwa mafanikio. Lengo kuu la chama cha SVP lilikuwa ni kuibua hofu miongoni mwa Waswisi kuhusu Uislamu. Hatimaye chama hicho chenye misimamo mikali kilifanikiwa katika kuwakinaisha Waswisi kupitisha sheria hiyo ya kibaguzi ya kupiga marufuku ujenzi wa minara ya misikiti. Daniel Streich ambaye ni kati ya wanasiasa vigogo wa chama cha SVP alikuwa mtu wa kwanza kuzungumzia hadharani suala la kupiga marufuku ujenzi wa minara ya misikiti. Alieneza harakati yake dhidi ya Uislamu kote Uswisi na hivyo kupanda mbegu za chuki na dharau dhidi ya Uislamu nchini humo. Alichochea kwa kiasi kikubwa hisia za watu dhidi ya ujenzi wa minara ya Misikiti na inasikitisha kuwa hatimaye alifanikiwa katika malengo yake hayo machafu. Lakini baada ya hatua hiyo, Uislamu kwa mara nyingine uliweza kuthibitisha uwezo wake mkubwa na misingi yake ya uhakika na hivyo kuzidi kuwatia kiwewe Wamagharibi. Daniel Streich aliyekuwa akiongoza harakati dhidi ya Uislamu sasa binafsi ni kati ya waliotambua ukweli kuhusu Uislamu na kuikumbatia dini hii tukufu. Fikra zake dhidi ya Uislamu hatimaye zilimpeleka hadi kufika katika nuru ya Uislamu na kumfanya afanye utafiti wa kina kuhusu dini hii ambayo ni njia kamili ya maisha. Alivutiwa sana na Uislamu katika utafiti wake hasa kuhusu mafundisho ya kimantiki na ya kivitendo maishani na hivyo akaamua kusilimu. Hivi sasa Daniel Streich ni mwalimu katika jeshi la Uswisi, mjumbe wa baraza la mji na zaidi ya yote ni Mwislamu mwenye kufungamana na mafundisho ya kidini na hakosi kuonekana msikitini. Anaisoma Qur'ani na kusimamisha sala tano kwa siku. Anaendelea kusema hivi kuhusu kusilimu kwake: "Uislamu umejibu kimantiki maswali muhimu niliyokuwa nayo kuhusu maisha. Nimepata majibu ambayo sikuwahi kuyapata katika Ukristo. Mimi nimepata uhakaika wa maisha katika Uislamu." Daniel Streich sasa anajuta kuhusu vitendo vyake vya huko nyuma dhidi ya Uislamu na sasa ana hamu kubwa ya kuona msikiti maridadi zaidi barani Ulaya unajengwa nchini Uswisi. Anasema anajitahidi kufidia aliyofanya wakati akiongoza kampenzi dhidi ya Uislamu. Leo kinyume na alivyokuwa huko nyuma anajitahidi kuunga mkono mikakati ya uhuru wa kuabudu na maisha ya pamoja kwa msingi wa imani ya wafuasi wa dini mbali mbali. Kuhusu hili Abdulmajid Aldai mkuu wa shirika la OPI ambalo hujishughulisha na kuimarisha maisha ya Waislamu Uswisi anasema: "Watu wa Ulaya wana hamu kubwa ya kuujua Uislamu. Aghalabu wanataka kuchunguza madai kuhusu iwapo kuna uhusiano kati ya Uislamu na ugaidi. Kimsingi wanafanya utafiti kama uliofanywa na Streich ambaye katika kielele cha harakati zake dhidi ya Uislamu aliisoma Qur'ani na kufanya utafiti zaidi kuhusu Uislamu. Alikuwa na hamu ya kukabiliana vilivyo na Uislamu lakini natija ilikuwa kinyume na hilo." Moja kati ya nukta za kipekee kabisa katika Uislamu ni kuwa mafundisho yake hayana kifani. Watu ambao wanaamua kuchukua hatua za kukabiliana na Uislamu baada ya kupata maelezo sahihi kuhusu dini hii hatimaye huvutiwa na kuifuata. Wao huutambua ukweli baada ya kufanya utafiti kuhusu masuala mbali mbali ya Kiislamu. Kwa hakika Uislamu ni dini ambayo imejengeka katika msingi wa mahitajio ya kifitra na kimaumbule ya mwanadamu. Ni kwa sababu hii ndio maana watu wengi ambao hufanya utafiti wa wazi na bila ya taasubi kuhusu dini hii huwa hawawezi tena kupinga ukweli wa dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu. Dkt. Garry Miller alikuwa mhubiri mashuri wa Kikristo nchini Canada. Katika utafiti wake alikusudia kutafuta kile alichodhani ni makosa katika Qur'ani na kutumia aliyopata katika vita dhidi ya Qur'ani na dini ya Kiislamu. Lakini natija ya utafiti wake ilikuwa kinyume na alivyokusudia. Dkt. Miller anasema: "Siku moja nilichukua Qur'ani na kuanza kuisoma. Awali nilidhani kuwa kutokana na kuwa Qur'ani ilishuka bara Arabu basi ingekuwa inaashiria sana kuhusu maisha ya eneo hilo. Laikini baadaye nilifahamu haikuwa hivyo. Hapo nilibadilisha lengo la kutafuta kile nilichodhani ni makosa katika kitabu hiki kitakatifu. Nilikuwa nikidhani kuwa kutokana na kuwa Qur'ani iliteremshwa karne 14 zilizopita basi ningeweza kupata makosa mengi ndani yake ambayo ningeyatumia katika kukabiliana na Waislamu. Lakini hatimaye baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu kuhusu Qur'ani, si tu kuwa sikupata makosa ndani yake bali pia nilijifunza mengi sana. Aya ambayo ilinipeleka katika kina cha fikra ni aya ya 82 ya Surat An-Nisaai isemayo: 'Je hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi." Mhubiri huyu Mkristo aliyesilimu anaendelea kusema: "Nukta iliyonishangaza sana ni hii kuwa katika Qur'ani Tukufu kuna sura kamili iliyopewa jina la 'Maryam' ambayo imempongeza na kumpa heshima mwanamke huyo mtukufu. Katika Injili hakuna sehemu yoyote ambayo Bibi Maryam ametunukiwa heshima kama ilivyo katika Qur'ani. Aidha Nabii Issa AS (Yesu) ametajwa mara 25 katika sehemu mbali mbali za Qur'ani katika hali ambayo Mtume Muhammad SAW ametajwa mara tano tu katika kitabu hicho kitakatifu." John Davenport, Mwingereza mtaalamu wa masuala ya Uislamu anasema hivi: "Qur'ani haina kasoro hata kidogo na haihitajii sahihisho lolote. Kwa miaka mingi makasisi wametuzuia kupata ukweli kuhusu Qur'ani Tukufu na adhama ya aliyeteremshiwa kitabu hicho, Mohammad SAW. Lakini kadiri tunavyosonga mbele tunazidi kutupilia mbali ujahili na taasubi tulizokuwa nazo na baada ya muda usio mrefu kitabu hiki kisicho na kifani kitawavutia walimwengu wote na kueneza taathira za kina kote duniani na kuwa mhimili wa fikra za watu wote duniani." http://kiswahili.irib.ir