Uislamu Chaguo Langu 20 + Sauti
Uislamu Chaguo Langu 20 + Sauti
0 Vote
166 View
Sikiliza Kuongezeka idadi ya Waislamu Marekani na hasa kuenea Uislamu miongoni mwa jamii za waliowachache katika nchi hii ni ukweli ambao umewavutia wengi. Mshikamano unaozidi kuimarika wa Waislamu ni jambo ambalo limepelekea nafasi yao ipate nguvu katika jamii ya Marekani kiasi kwamba weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa hivi sasa Uislamu ni sehemu ya jamii na utamaduni wa Marekani. Wapenzi wasikilizaji karibuni kujiunga name tena katika makala nyingine ya 'Uislamu Chaguo Langu' ambapo tutamuangazia Mmarekani aliyesilimu Bi. Monica Waite. @@@ Monica Waite ni Mmarekani aliyesilimu na sasa yeye ni mwanaharakati wa 'Harakati ya Kukalia Wall Street' yaani Occupy Wall Street Movement na alisilimu mwezi Januari mwaka 2012 akiwa safarini nchini Iran. Monica Waite aliwahi kuhudumu katika jeshi la Marekani kwa muda wa miezi sita. Baada ya kufanya uchunguzi kuhusu dini mbali mbali aliamua kuikumbatia dini tukufu ya Kiislamu kwa kutamka shahada mbili na kisha kuchagua jina la 'Nargis'. Anasema hivi kuhusu alivyosilimu: 'Kwa muda kuna swali ambalo lilikuwa likinishughulisha akilini na hili ni kuwa, ni kwa nini nchini Marekani Ukristo hauzingatii mustakabali wa maisha yetu? Katika nchi za Magharibi tunaambiwa kuwa tuwe na nguvu, tupate kazi nzuri, tuishi maisha mazuri n.k lakini hatufahamiswhi lengo la haya yote. Hali hii iliendelea hadi nilipopata fursa ya kuisoma Qur'ani wakati nikiwa chuo kikuu. Baada ya kukisoma kitabu hicho kitukufu nilihisi kuwa kwangu Mkristo kulikuwa kumefika ukingoni. Ukristo haukuweza kukidhi mahitaji yangu na kuniainishia mustakabali. Nilipoitembelea Iran nilipata fursa ya kutafakari kuhusu maisha na mustakabali wangu. Katika Uislamu nilipata jibu nililokuwa nikilitafuta kuhusu lengo kuu la maisha na ni kwa nini tunapaswa kuishi maisha bora." Kuzingatiwa haki za wanawake ni suala ambalo limeifanya dini ya Kiislamu iwe bora zaidi kuliko dini zingine zote. Uislamu umeangamiza hisia zote za ubora wa kikabila, kirangi, kijinsia na kifedha. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu wanaadamu wote wakiwemo wanawake na wanaume, matajiri na masikini, weupe na weusi n.k wote ni sawa. Katika Uislamu kigezo pekee cha ubora ni takwa, thamani za kimaanawi na fadhila za kiakhlaqi. Allah SWT katika Qur'ani Tukufu Surat al H'ujuraat aya ya 13 anasema: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari." Hivi sasa Bi. Waite anaamini kuwa sheria za Kiislamu na nidhamu maalumu katika dini hii kuhusu wanawake ni jambo ambalo limehifadhi thamani za mwanamke na kumuokoa kutoka katika utumwa. Anasema Uislamu sasa unamuongoza mwanamke katika hali yake ya kweli. Bi Waite anaongeza kuwa: "Moja ya masuala yaliyonipelekea nifanye utafiti kuhusu Uislamu ni tabia nzuri za Waislamu hasa Wairani namna wanavyoamiliana na wanawake. Katika zama ambazo nilikuwa nakihudumu kama askari wa jeshi la Marekani, nilijifunza kuhusu Iran kwa sababu za kikazi. Kwa hivyo nilifanya utafiti mwingi kuhusu Iran na hapo nikagundua kuwa muamala wa kila siku wa mwanaume Muirani na mwanamke ni tofauti na tulivyokuwa tukifahamu katika nchi za Magharibi." Anaendelea kusema: "Nilifanya utafiti kuhusu sababu ya kuheshimiwa mwanamke nchini Iran na nikafikia natija hii kuwa wanawake Iran wanaheshimiwa kwa sababu Uislamu unampa hadhi na heshima mwanamke." Mmarekani huyu aliyesilimu ambaye pia yuko katika 'Harakati ya Kulalia Wall Street' inayopinga dhulma za mfumo wa kibebaru anasema hivi kuhusu hali ya kisiasa na kijamii nchini Marekani: "Harakati zinazoshuhudiwa Marekani hivi leo ni tone tu na katika siku za usoni tutashuhudia matukio makubwa na mapana zaidi. Watu wa Marekani wamechoshwa na sera za viongozi wa nchi hii ambao wanawatumia wananchi kama ngao ya kufikia malengo yao ya kujitanua na kibeberu. Malalamiko ya wananchi wa Marekani yanabainishwa kwa njia mbali mbali." Uislamu ni mfumo sahihi wa kuishi na kigezo bora cha maisha. Lakini katika kipindi kirefu cha historia Wamagharibi wamekuwa wakitumia mbinu mbali mbali za wazi na za nyuma ya pazia kuupiga vita Uislamu. Ni kwa sababu hii ndio tumekuwa tukishuhudia tuhuma zikitolewa mara kwa mara dhidi ya Uislamu. Upotoshaji huu umepelekea watu wengi wa nchi za Magharibi kuwa na taswira isiyo sahihi kuhusu Uislamu. Mmarekani aliyesilimu Bi. Monica Waite anaashiria pia njama za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi za kueneza habari zinazopotosha ukweli kuhusu Uislamu na kusema: "Baada ya kuutambua uhakika kuhusu Iran na Uislamu, nilifahamu namna vyombo vya habari vya Kimagharibi vinavyopotosha ukweli kuhusu sura nzuri ya Uislamu. Kwa hivyo nimeamua kusimama kidete na kukabiliana na njama hizi. Hapa baada ya kuikubali dini tukufu ya Kiislamu natangaza kuwa nitatumia uwezo wangu wote kufanya utafiti na kuusoma Uislamu." Herbert George Wells mwandishi na mtafiti Muingereza anasema hivi: "Uislamu ndio dini pekee ambayo kila mwanaadamu mwenye heshima anajifaharisha kuwa mfuasi wake....ndio dini pekee ambayo inaenda sambamba na maumbile na inaenda sambamba na ustaarabu wa mwanaadamu. Mafunzo ya Kiislamu yamepelekea kuibuka ustaarabu uliokuwa bora kuliko staarabu zingine hasa katika masuala ya kutetea uadilifu na kupinga dhulma. Kwa hakika kuongezeka idadi ya watu wanaovutiwa na Uislamu katika nchi za Magharibi ni jambo linaloashiria kuwepo malalamiko dhidi ya umaada, ubepari na utovu wa maadili." Aidha idadi kubwa ya watu katika nchi za Magharibi wamechoshwa na hali ya kutokuwepo umaanawi katika jamii zao. Kuhusu suala hili, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema njia pekee ya kumuokoa mwanaadamu kutoka katika matatizo ya zama zetu hizi ni kurejea katika dini pamoja na imani. Anaendelea kusema kuwa: "Iwapo mwanaadamu atafika katika kilele cha sayansi na ustawi wa kimaada lakini wakati huo huo awe anatawaliwa na na watu madhalimu na wanaotumia mabavu, watu wenye nguvu wawe wanakandamiza haki za walio dhaifu, nuru ya maarifa na ubinaadamu itoweke duniani na hadaa ienee; kwa hakika wanaadamu watakuwa katika ujahili na upotofu na mwanaadamu hataweza kuokoka isipokuwa tu pale atakapotekeleza mafundisho ya Kiislamu ambayo ni yenye kuponya na yaliyo na itibari ya daima." http://kiswahili.irib.ir