Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (10)

Bismillahir Rahmanir Rahim Kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kumkabidhi Mola Mlezi kazi zetu, hakuna maana ya kwamba, mwanaadamu akae na kubweteka na kuacha kunufaika na suhula za kimaumbile zilizoko kwa ajili ya kufikia malengo yake. Kutawakali kwa Mwenyezi Mungu hakuna maana ya kutozishughulisha suhula zilizoko ambazo kimsingi ziko kwa ajili yetu. Mja muumini, hutawakali kwa Mwenyezi Mungu na hufadhilisha kumtegemea Mwenyezi Mungu Muumba badala ya kuwategemea asiyekuwa Yeye. Mwenyezi Mungu anazungumzia suala la kutawakali kwake katika Surat ya Aal Imran aya ya 159 kwa kusema: "Na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea." Katika aya hii Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume Wake kwamba, baada ya kukata shauri kwa maana kwamba, baada ya kutathmini hali ya mambo na jambo lenyewe na kuandaa suhula za lazima, basi ifanye kazi hii hali ya kuwa unatawakali na kumtegemea Mola Muumba. Ayatullah Murtadha Mutahhari msomi mtajika katika ulimwengu wa Kiislamu anasema: "Mafuhumu ya kutawakali ni mafuhumu na fasili hai. Yaani kila mahala ambapo Qur'ani Tukufu inataka kumfanya mwanadamu afanye kazi na kumuondolea woga na hofu, humwambia kwamba, tawakali kwa Mwenyezi Mungu na umtegemee Yeye. Songa mbele na ufanye hima." Mafuhumu na fasili ya kweli ya kutawakali ni hii kwamba, mwanadamu anapaswa kumfanya Mwenyezi Mungu Muumba kuwa tegemeo na kiegemeo chake cha pekee na kuwa na imani nae kamili na wakati huo huo atake msaada na kutumia suhula na nyenzo zote za kidunia ambazo ni nyenzo za kimaada kwa ajili ya kuboresha maisha yake. Na mtu mwenye kutawakali anapaswa kufahamu kwamba, nyenzo zote za kimaada ziko kwa ajili ya mwanadamu kwa mujibu wa mipango na irada ya Mwenyezi Mungu. Katika mazingira kama haya kutawakali kwa Mwenyezi Mungu hakuwezi kuwa sababu na hoja ya kuacha kufanya kazi na hivyo kuukumbatia uvivu. Katika Qur'ani Tukufu tunasoma kisa cha Dhul Qarnein na kuona jinsi gani alivyotumiwa nyenzo zote za kimaada alizopatiwa na Mwenyezi Mungu katika kupambana na dhulma na uonevu. Hata alipofanikiwa kujenga kizuizi cha chuma baina ya watu na maadui alisimama na kusema: "Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu Mlezi. Na itapofika ahadi ya Mola wangu Mlezi atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu Mlezi ni kweli tu". Wakati mwingine mtu huandaa mipango kwa ajili ya kazi fulani na kuchunguza vizuri engo na pande za kazi hiyo na kidhahiri hupata natija kwamba, hakuna kizuizi cha kumfanya ashindwe kuifanya vizuri kazi hiyo na kufikia malengo aliyoyakusudia iwe ni kazi ya biashara au kazi ya ujenzi na kadhalika. Hata hivyo hutokea tukio dogo tu ambalo huja kuvuruga mahesabu yake yote na hivyo kuifanya kazi yake kutokuwa na natija. Hii inatokana na kuwa, elimu ya mwanadamu ina mipaka na mwanadamu hana habari na matukio au mishkili tarajiwa. Fauka ya hayo, wakati mwingine mwanaadamu anapoamua kufanya kazi fulani au anapokata shauri kuiacha huwa hana habari ya maslahi yaliyoko katika kazi hiyo. Kwa mtazamo wa dini, mwanaadamu hukabiliwa na hakika yenye matumaini nayo ni kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye mtawala mutlaki wa ulimwengu na hekima na elimu isiyo na kikomo iko kwake. Mola Muumba ana uwezo wa kufanya kazi zote na vile vile ana ufahamu juu ya maslahi ya kweli ya waja wake. Hatua ya mja ya kutawakali kwa Mwenyezi Mungu mwenye sifa hizi humfanya ujudi wake ufungamane na nguvu isiyo na kikomo. Mja anayetawakali kwa Mwenyezi Mungu hushuhudia na kuona nguvu za Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu katika kazi na mambo yake na hunufaika na nguvu maalumu. Marhumu Allama Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai mfasiri mkubwa wa Qur'ani Tukufu anaandika hivi kuhusiana na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu: "Wakati mwingine mwanadamu akiwa nia ya kufikia lengo lake fulani, huingia katika medani na kuona kuwa anayo mahitaji yote ya lazima, lakini baadhi ya sababu za kiroho kama kuwa na irada inayotetereka, woga, pupa na tajiriba ndogo huingia baina yake na kazi husika. Kama mtu atatawakali kwa Mwenyezi Mungu katika mazingira kama haya, irada yake huwa na nguvu, azma yake huwa thabiti na vizingiti vya kiroho huondoka. Kwani mwanadamu akiwa na hali ya kutawakali kwa Mwenyezi Mungu huungana na chemchemi ya mambo yote yaani Mwenyezi Mungu na kwa muktadha huo, wasi wasi na vishawishi hutoweka." Kutawakali kunamfanya mtu awe na ujasiri wa kufanya jambo na kwa hatua hiyo hufanikiwa kuondoa vikwazo na viziuzi vyote viwe vya kifikra au kimuamala. Mtu mwenye kutawakali kwa Mwenyezi Mungu sambamba na kutumia nyenzo na suhula zilizoko katika maisha kwa ajili ya kazi na kufanya hima ili kufikia lengo lake, huwa na imani kwamba, Mwenyezi Mungu atamsaidia kufikia lengo lake kupitia suhula au kupitia njia nyingine ambayo mwanadamu hawezi kuifikiri wala kuitasawari. Kwa msingi huo tunapaswa kusema kuwa, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu hakuna maana ya mtu kujishughulisha tu na ibada, dua na kunong'ona na Allah na hivyo kuacha kufanya kazi. Imepokelewa kwamba, "siku moja Bwana Mtume SAW alishuhudia kikundi fulani cha watu ambacho hakikuwa kikijihusisha na kazi. Mtume akawauliwa: Mnaendesha vipi maisha yenu? Watu wale wakamjibu kwa kusema, sisi ni watu wanaotawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Baada ya Bwana Mtume SAW kusikia kauli yao hiyo akawaambia: Nyinyi sio mnaotawakali kwa Mwenyezi Mungu bali nyinyi ni mzigo katika jamii." Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. http://kiswahili.irib.ir