Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (7)

Bismillahi Rahmanir Rahim Imam Jafar Sadiq AS anasema kuwa, siku ambayo Nabii Adam AS alipotolewa na Mwenyezi Mungu katika pepo na kuletwa katika mgongo wa ardhi alikuwa akihitajia chakula na maji, hivyo alishauriana na Malaika wa Wahiy yaani Jibril na kutaka amsaidie. Malaika Jibril alimpa muongozo Nabii Adam AS namna hii: "Ewe Adam, kama unataka kudhamini mahitaji yako, kuwa mkulima na jishughulishe na kilimo." Aidha tukirejea historia ya Manabii wengine kama Nuhu, Mussa, Daud na kadhalika wote walikuwa wakijishughulisha na kazi fulani ili waweze kudhamini mahitaji yao ya kimaisha na hawakubweteka na kungoja vya bure kutoka kwa watu kutokana tu na kuwa wao ni waja wateule wa Mwenyezi Mungu. Mafundisho ya Uislamu, sira pamoja na mwenendo wa Bwana Mtume SAW na Ahlu Bayt zake unabainisha uhakika huu kwamba, Uislamu ni mshika bendera wa thamani ya kazi na wafanyakazi; na dini hii inathamini mno kazi na watu wanaofanya kazi na kutokwa na jasho kwa ajili ya kutafuta riziki ya halali. Sio tu kwamba, Bwana Mtume SAW yeye na familia yake walikuwa watu wa hima na kufanya kazi, bali alikuwa akiwashajiisha pia watu wengine kufanya kazi na kujituma kwa ajili ya kudhamini mahitaji yao ya maisha. Waja hao wema wa Mwenyezi Mungu wakiwa na lengo la kufikia malengo yao na ushindi mkubwa, sambamba na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu muweza huku wakiomba auni na msaada Wake, hawakughafilika kamwe na mipango, tadbiri na suala la kufanya kazi. Kuomba dua na kutawassali kwao, hakukuwafanya watu hawa wa Mwenyezi Mungu kuacha kufanya hima na bidii kwa ajili ya kutafuta riziki. Hii inarudi na kukosoa fikra potofu za wale wanadai kwamba, riziki inatoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo kufanya hima na kujituma au kufanya uvivu na kubweteka hakuwezi kuongeza au kupunguza riziki ambayo tayari mja amekadiriwa na Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume SAW alikuwa akibusu mikono ya kibarua na alikuwa akichukizwa mno na watu wavivu, wenye kubweteka na wasiofanya kazi. Siku moja Bwana mmoja wa Madina aliyejulikana kwa jina la Sa'ad alikwenda kumpokea Mtume SAW na kisha wakapeana mikono. Wakati wanapena mikono, Bwana Mtume SAW alihisi kwamba, mkono wa Sa'ad ni mgumu, uliokomaa na kutoa sugu. Mtume SAW akamuuliza Sa'ad umefanya nini hata mikono yako imekomaa na kutoa sugu namna hii. Sa'ad akamjibu Bwana Mtume SAW kwa kusema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kazi yangu inahusiana na kamba na beleshi, mimi ninafanya sana kazi kwa kutumia beleshi, kwani nalazimika kufanya hivyo ili nidhamini kipato cha maisha ya familia yangu, ndio maana mikono yangu imekomaa na kuota sugu. Baada ya Mtume SAW kusikia maneno hayo alichukua mikono ya Sa'ad akaitazama na kuibusu kisha akasema; hii ndio mikono ambayo haitounguzwa na moto wa Jahanamu. Baadhi ya vijana wamekuwa wakiendekeza tabia ya uvivu badala ya kujishughulisha na kazi za kutafuta riziki. Matokeo ya vijana kuzurura mitaani na kukaa vijiweni bila ya kazi huwatumbukiza katika mambo mabaya ya wizi na uraibu wa madawa ya kulevya. Aidha utafiti unaonyesha katika baadhi ya nchi, baadhi ya vijana wamekuwa wavivu kwa sababu ya ruzuku inayotolewa na serikali. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu haijuzu kwa Muislamu kutofanya kazi kwa kisingizio cha kuyaweka maisha yake kuwa wakfu kwa ajili ya kufanya ibada tu. Badala ya mtu kuwa omba omba na kujidunisha au kujidhalilisha kwa watu, anapaswa kufanya kazi yoyote ile madhali tu haikiuki misingi na maadili ya Uislamu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu hakuna kazi duni na dhalili kama wanavyoamini baadhi ya watu. Kazi yoyote yenye kukidhi mahitaji ya jamii au inayoleta faida inachukuliwa kuwa ni nzuri, ilimuradi tu anayeifanya aifanye kwa njia nzuri, na kama inavyotakiwa na mafundisho ya Uislamu. Kuna baadhi ya watu wanazidunisha baadhi ya kazi, lakini Mtume SAW anatufundisha kuwa heshima na hadhi ya mtu imefungamana na yeye kufanya kazi, kazi ya aina yoyote ile isipokuwa kazi ambazo zimeharamishwa kama kufanya biashara ya pombe na kadhalika. Hata hivyo katika suala zima la kufanya hima, kujituma na kufanya kazi, wanadamu wana mitazamo tofauti kuhusiana na hili. Baadhi ya watu wanaona kuwa, maisha yanaishia katika dunia hii hii ya kimaada. Hivyo watu wenye itikadi kama hii hufanya hima na kujituma huku hima na idili yao yote wakiielekeza tu hapa duniani. Lakini kuna kundi la pili ambalo lenyewe linaamini kwamba, dunia hii ni mapito tu na maisha ya kweli ambayo yana saada ya kweli ni huko Akhera. Hivyo wakiwa hapa duniani watu hawa hujituma na kufanya hima ili wakapate maisha bora yenye saada na ufanisi wa kweli kesho akhera. Watu hawa hutumia suhula zote hapa duniani kwa ajili ya kupata ukamilifu wa maanawi. Kwa muktadha huo kazi ni hitajio la kawaida la mwanadamu. Wakati huo huo, dini na mafundisho yake yanamshajiisha mwanadamu katika hilo. Kama tulivyoashia katika vipindi vyetu vilivyotangulia, lengo aali la mwanadamu hapa ulimwenguni kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu ni kufanikiwa kufikia daraja ya uja na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu jambo ambalo humfanya apate radhi za Mola Muumba. Kwa mtazamo wa Uislamu kudhamini mahitaji ya maisha ni kumfanya mwanadamu aweze kufanya harakati kuelekea upande wa kufikia lengo hili. Ili mwanadamu aweze kuwa na utulivu na hivyo kufanya ibada pasina ya wasi wasi, bila shaka kimaumbile anahitaji maji, chakula, nyumba na hawaiji nyingine za kimaisha na haya yote hayapatikani bure bure bila ya kuweko hima, bidii na kufanya kazi. Hivyo basi, haki ya wazi ya mwanadamu ni hii kwamba, anapaswa kujishuhughulisha na harakati za kukidhi hawaiji na mahitaji yake ya kimaada; hata hivyo hii sio njia pekee ya kufikia ukamilifu wa kimaanawi. Hivyo kufanya kazi kunafukuza uvivu na hali ya kubweteka na hivyo kuleta nishati na uchangamfu katika mwili wa mwanaadamu. Aidha kufanya kazi humuandalia mja mazingira ya kupata saada ya kesho Akhera. Jamii ya watu wavivu ni jamii ambayo hubakia nyuma kimaendeleo na hivyo kukabiliwa na matatizo chungu nzima. Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, kufanya kazi ni wenzo bora kabisa wa kumletea mwanaadamu uzima wa kifikra na kimwili na hivyo kumfanya mtu kuwa mwenye harakati. Fauka ya hayo, kazi huweza kutatua matatizo ya kiuchumi ya mtu na familia yake na hivyo kuleta utulivu katika familia na jamii kwa ujumla. http://kiswahili.irib.ir