Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (9)
Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (9)
0 Vote
111 View
Bismillahir Rahmanir Rahim Kama tulivyosema katika makala zetu zilizotangulia, katika mtazamo wa Uislamu, itikadi ni mambo ambayo yana nafasi muhimu katika harakati za maisha ya mwanadamu ikiwemo miamala yake ya kiuchumi. Ni kwa muktadha huo ndio maana kila Mwislamu huboresha harakati na shughuli zake za kiuchumi katika fremu ya mafundisho ya dini; kwani itikadi ni msingi wa mambo yote ya kimaisha. Ni kwa msingi huo ndio maana malengo ya mfumo wa kiuchumi wa Kiislamu yako kwa ajili ya kuimarisha thamani na kumfanya mwanadamu afikie katika saada na ukamilifu wa kweli. Kazi na kufanya hima nako kukiwa ni aina ya harakati ya kiuchumi, kuna nafasi muhimu katika kuandaa mazingira ya lazima kwa ajili ya ustawi na ukamilifu wa mwanadamu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika maandiko na matini za kidini na vile vile utendaji wa mawalii na viongozi wa dini kazi inahesabiwa kuwa harakati matulubu na inayofaa na imekokotezwa na kutiliwa mkazo mno; kiasi kwamba, mbali na faida za kidunia na kuichumi ina thawabu na ujira kwa ajili ya kesho Akhera. Licha ya kuweko msisitizo mkubwa namna hii, lakini kuna baadhi ya watu wanadai kwamba, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu au kuwa na itikadi kwamba, riziki inatoka kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuja katika maarifa ya Kiislamu kunakinzana na maelekezo na maagizo yaliyotolewa kuhusiana na hima na suala la kufanya kazi. Kwa mfano katika aya ya 6 ya Surat Hud Mwenyezi Mungu anasema: "Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. " Ikiwa Mwenyezi Mungu amedhamini riziki kwa ajili ya viumbe, basi kwa nini watu wahangaike na kutaabika wakifanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kutafuta riziki? Katika kubainisha shubha hii Shahidi Ayatullah Murtadha Mutahhar mwanafikra wa Kiislamu anasema: "Endapo tutamfahamu Mwenyezi Mungu kama inavyostahiki na tukatambua sifa Zake aali, wakati huo tutadiriki kwamba, dhamana ya Mwenyezi Mungu kuwapatia riziki waja wake, haikinzani na taklifu pamoja na haki za mwanadamu. Mwenyezi Mungu amejitaja katika Qur'ani kwamba, Yeye Ndiye mtoaji riziki, lakini wakati huo huo akawataka watu wajitume, wafanye hima na kufanya kazi. Hii kwamba, Mwenyezi Mungu ni mtoaji riziki maana yake ni kuwa, kila kiumbe anapaswa kutumia suhula zilizoko kwa ajili ya kumrahisishia mambo yake katika njia ya kutafuta riziki. Kwa mfano wakati mmea unapofyonza maji na madini yaliyoko katika udongo ardhini kwa njia ya mizizi au wanyama wanapojishughulisha na uwindaji kwa ajili ya kutafuta chakula chao, bila shaka uwezo huu ni dhihirisho la kwamba Mwenyezi Mungu ni mtoaji riziki. Mwenyezi Mungu amemjaalia kila kiumbe hai kuwa na raghba ya kufuata na kutafuta anayoyahitaji na kudhamini mahitaji yake kupitia hima na raghba hii aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu." Aidha katika kuendelea kufafanua utoaji riziki wa Mwenyezi Mungu, Ustadh Mutahhari anasema: "Hima inayofanywa na mwanadamu kwa ajili ya kupata haki zake na kustafidi nazo, hii nayo ni aina fulani ya dhihirisho la utoaji riziki wa Mwenyezi Mungu. Katika Qur'ani Mwenyezi amebainisha kwamba, rizki ya kila kiumbe inatoka kwake, yaani kama dhamana ya riziki hiyo isingekuweko, basi ile raghba na hamu ya kufanya harakati kwa ajili ya kutafuta riziki nayo isingelikuweko katika ujudi wa viumbe. Mwanadamu kwa upande wake pia asingekuwa na hamu ya kutaka kulinda haki zake. Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu suhula nyingi zaidi kutokana na kuwa yeye ni kiumbe bora miongoni mwa viumbe wengine; hasa kutokana na kutunukiwa neema ya akili. Ni kutokana na uhakika huo, ndio maana mwanadamu anapaswa kutumia nguvu zake zote, kipaji na uwezo alionao kwa ajili ya kutafuta riziki na hivyo kujidhaminia mahitaji yake maishani." Hivyo basi Mwenyezi Mungu ni mtoaji riziki, lakini utoaji riziki huo haukinzani na harakati ya kimaumbile na sheria zinazohukumu ulimwengu ambazo ameziweka Mwenyewe. Moja ya sheria hizo zinazotawala ulimwenguni ni kwamba, suhula na nyenzo nyingi huandaliwa kwa viumbe sambamba na hima na bidii. Kwa maana kwamba, anayefanya hima na bidii zaidi ndiye ambaye hunufaika zaidi na anayefanya uvivu hunufaika kwa kadiri ya uvivu wake. Mwanadamu kama walivyo viumbe wengine naye hunufaika na suhula zilizoko humu duniani kwa sharti la kuweko hima na kufanya kazi. Hivyo basi kustafidi na suhula kama akili na nguvu za mwili na kifikra kwa ajili ya kudhamini mahitaji na hawaiji ni ishara ya kwamba, riziki inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama tulivyosema Bwana Mtume SAW pamoja na Ahlul Bayt zake walitilia mkazo mno suala la kazi na kufanya hima. Hilo lilionekana wazi katika maneno na amali zao na walikuwa amilifu katika kutafuta riziki. Sasa na tuzingatie kisa kifuatacho: Siku moja Imam Mussa al Kadhim AS alikuwa amezama katika kazi ya kulima. Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Ali Bin Abi Hamza alipita mahala hapo na alipomuona Imam Kadhim yuko katika hali ya kulima akamuuliza kwa mshangao: Kwa nini kazi hii huikabidhi kwa mtu mwingine? Imam akamjibu kwa kumwambia: Kwa nini niikabidhi kazi kwa watu wengine? Ilhali watu ambao ni wabora kuliko mimi daima walikuwa wakijishughulisha na kazi kama hii? Bwana yule akamuuliza Imam: Maulana wangu, unawazungumzia watu gani? Imam Kadhim AS akamjibu Abu Hamza kwa kumwambia: Mtume wa Mwenyezi Mungu, Imam Ali AS na na mababa na mababu zangu wote. Kimsingi kazi na kujishughulisha na kilimo ni suna na ada za Mitume, Mawasii wa Mitume na waja wateule na wastahiki wa Mwenyezi Mungu. Kama tulivyosema katika makala iliyopita, baada ya kubaathiwa na kupewa Utume pia, Muhammad SAW hakuacha kufanya kazi zake na katu hakuishi maisha kama ya Wafalme na mabwanyenye. Kazi yake ya Utume ilikuwa na mazonge mengi lakini haikumzuia kufanya kazi zake nyingine zinazohusu maisha yake. Akiwa mjini Madina, Mtume SAW aliitumia sehemu kubwa ya umri wake kwa ajili ya kufikisha risala ya Mwenyezi Mungu na kujihami dhidi ya maadui. Pamoja na hayo yote, hakuacha kutumia hata fursa ndogo aliyoipata kwa ajili ya kufanya kazi na hima kwa ajili ya maisha yake na familia yake. Imekuja katika historia ya maisha ya Imam Ali AS kwamba, kila mara alipokuwa akikamilisha kazi ya Jihadi, alikuwa akijishughulisha na kazi ya kutoa hukumu au kufundisha na alikuwa akifanya kazi nyingine kama kulima na kuchimba visima. Imam Ali AS alichimba kisima katika eneo moja magharibi mwa mji wa Madina kisima ambacho kilikuwa kikitoa maji mengi. Aidha akiwa katika eneo hilo Imam Ali alikuwa akijishuhghulisha na kilimo na alikuwa na bustani nyingi katika eneo hilo. Ilikuwa vigumu mno kufanya kazi katika eneo hilo hasa kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma katika eneo hilo lililojulikana kwa jina la Yanba'a. Ndio maana hakuna mtu ambaye alikuwa yuko tayari kujishughulisha na kilimo katika eneo hilo. Lakini Imam Ali AS aliinunua ardhi hiyo ambapo ugumu wa kazi katu haukumfanya aache kufanya hima na bidii katika kazi yake ya kilimo Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. http://kiswahili.irib.ir