Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (12)
Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (12)
0 Vote
78 View
Bismillahir Rahmanir Rahim Makala hii inabainisha na kutupia jicho baadhi ya faida za kijamii na kiuchumi zinazotokana na kufanya kazi. Kujituma na kufanya kazi ni moja ya sababu muhimu za ustawi wa kiuchumi na kijamii wa jamii. Hii leo nafasi ya mtaji wa mwanadamu au nguvu kazi katika kukua na kupatikana maendeleo ya kiuchumi ni miongoni mwa mambo muhimu na ya kimsingi mno katika uchumi mkubwa. Kimsingi kujituma na kufanya kazi ni uga wa nguvu na uwezo wa mataifa. Kadiri taifa fulani litakavyojituma katika uga wa hima na kufanya kazi ndivyo mazingira ya kufikia ustawi na maendeleo yatakavyoandaliwa zaidi. Imam Ali bin Abi Talib AS mmoja wa Maimamu watoharifu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW anasema: "Wenye kufanya hima hufanikiwa kufikia ustawi na maendeleo, kuliko wasomi wanaokaa bila kazi." Madhumini ya Imam Ali AS ni kuwa, jamii hufanikiwa kufikia ustawi na maendeleo kwa wenye vipawa na wasomi wa jamii husika kufanya kazi kwa hima na jaddi, kwani ujuzi na elimu huwa na faida katika medani ya kazi na hivyo natija yake kuonekana na kudhihiri. Kama tulivyotangulia kusema, msingi wa maisha umesimama juu ya hima na kufanya kazi na uzima wa kiroho na kimwili wa mtu na jamii nao unapatikana kwa kuwa na maisha na uchumi salama. Kwa msingi huo katika mkusanyiko salama, wanajamii wote kila mmoja anapaswa kuwa na hisa yake katika uga wa uzalishaji bidhaa na utoaji huduma na kuwa na nafasi muhimu katika ushiriki wa masuala ya kijamii. Kadiri roho na moyo wa hima na kufanya kazi utakavyokuwa imara na madhubuti katika jamii, ndivyo ambavyo uwanja wa kuongezeka uzalishaji huandaliwa na matokeo yake kuwa ni kukua zaidi uchumi jambo ambalo bila shaka lina manufaa makubwa kwa jamii yoyote ile. Katika uga wa mtu binafsi, kuna mlolongo wa mahitaji ya mtu kuanzia chakula na mavazi hadi kupata daraja katika jamii ambapo mambo haya humsukuma mtu kujituma na kuwa na bidii katika kufanya kazi ili aweze kukidhi mahitaji yake ya kimaisha. Katika uga wa kijamii pia hutokea anga ya ushindani wa wanajamii kwa ajili ya kujipatia kipato, ushirikiano wa wanajamii na hivyo kukuza roho ya kazi hima na bidii katika jamii. Tunashuhudia leo katika jamii zetu, mtu ambaye hana kazi na ambaye anazurura na kuranda randa tu mitaani, hana hadhi wala heshima kwa majirani na hata katika jamii anayoishi. Lakini mtu mwenye kazi yake huheshiwa na kuonekana mtu mwenye heshima na hadhi katika jamii. Utamaduni na mafundisho ya Uislamu yanatoa wito wa kuweko ushirikiano wa pamoja wa wanajamii na hima za pamoja na yanawataka wanajamii kufanya hima na bidii katika kazi na kutofikiria maslahi yao binafsi bali kutanguliza mbele maslahi ya wote. Natija ya kuweko mtazamo kama huu huleta roho na moyo wa mfungamano katika jamii. Kwa mtazamo wa Uislamu, wananchi ni nguzo kuu ya ustawi na maendeleo; hasa kwa kutilia maanani kwamba, kila mmoja ana uwezo wa kifikra na kipaji cha aina yake ambacho kinaweza kutumiwa katika nyuga mbalimbali kwa ajili ya kufikia ustawi na maendeleo. Kwa kuzingatia kwamba, wanadamu ni viumbe wa kijamii hawana budi kuwa na ushirikiano baina yao ili waweze kufikia katika malengo yao ya kimaada na kimaisha. Ukweli wa mambo ni kuwa, kila mwanaadamu ananufaika na kustafidi na matunda ya mwenziwe na hakuna mtu anayeweza kuishi katika jamii bila ya kumtegemea mwenzake hata kama atakuwa na utajiri wa kutupa; kwani ili aweze kufanyiwa kazi fulani hana budi kumuajiri mtu. Hivyo tunaweza kusema kuwa, mtu anapaswa kuwa yuko kwa ajili ya jamii kabla ya kuwa yuko kwa ajili yake. Ustadh Shahidi Murtadha Mutahhar, mwanafikra mtajika wa Kiislamu anasema kuwa, kimsingi kazi ni wadhifa wa kijamii na jamii ina haki kwa mtu. Matumizi na vitu anavyotumia mtu ni natija ya kazi za wengine. Nguo tunazovaa, chakula tunachokula, viatu tunavyovivaa na nyumba tunazoishi, kadiri tunavyotazama tunaona kuwa ni natija ya kazi za watu wengine." Mwisho wa kunukuu. Kwa msingi huo kazi ina taathira kubwa na muhimu mno katika kuimarisha mtandao wa mahusiano ya wanadamu na unamuunganisha mwanadamu na jamii. Mafungamano ya kijamii ni injini ya hima na harakati ya wanajamii kwa ajili ya ustawi na malengo. Hivyo basi hima na kazi inahitaji kukuza shauku na msukumo wa kijamii na kuhisi kuwa na masuuliya kwa wengine. Kwa hakika kila mtu ana jukumu na masuuliya mkabala na jamii; na jamii nayo ina masuuliya kwa mtu huyu na inapaswa kumdhaminia mahitaji yake. Huu uhusiano wa pande mbili unalenga mfungamano baina ya mtu na jamii na kwa msingi huo mfungamano wa kijamii ambao ni muhimu nao hupatikana. Kuandaliwa nafasi za ajira na kazi kwa ajili ya matabaka yote ya jamii hupekekea kupatikana uadilifu wa kijamii. Kwa mtazamo wa Uislamu, uadilifu maana yake ni kutoa fursa sawa kwa watu wote. Endapo hali ya upatikanaji kazi na ajira itakuwa mbaya, kigezo cha ushiriki wa kiuchumi kikawa dhaifu sambamba na ukosefu wa kazi au kutofanywa kazi kama inavyotakiwa, uadilifu wa kijamii hauwezi kupatikana. Miongoni mwa mambo yanayokwamisha ustawi na maendeleo ya jamii ni uvivu, uraibu wa madawa ya kulevya na uhalifu. Hatua ya Uislamu kuweka uhuru wa kiuchumi na kushajiisha kufanya kazi ni jitihada zake za kujaribu kuzuia kutokea tofauti za kimatabaka katika jamii. Hii leo masuala ya kazi na ajira ni miongoni mwa masuala muhimu na yanayozingatiwa na wakurugenzi wa masuala ya kiuchumi wa nchi mbalimbali. Licha ya kuwa maendeleo ya kiteknolojia yamekuja na kuchukua kwa kiwango kikubwa kazi za mwanadamu, lakini tunapaswa kusema kuwa, teknolojia yenyewe ni natija ya kazi na ubunifu wa mwanadamu. Endapo mazingira ya kazi hayatoandaliwa basi watu wenye vipaji hawatoweza kuleta uwanjani uwezo wao na kustafidi na suhula zilizoko kwa ajili ya ustawi na maendeleo. Hima na kufanya kazi ni dhamana ya kubakia na kuongezeka kwa mali na mtaji. Endapo mwanadamu atafanya hima na kazi na kustafidi na mtaji wa kimaada, mbali na kuhifadhi mtaji wake, hatua hiyo hupelekea kuongezeka kwa mali na mtaji wake; lakini kama hatofanya kazi na kutoizungusha mali yake, hatua kwa hatua gharama za maisha hupelekea mtaji wake kumalizika. Siku moja Imam Jafar Sadiq AS alimuuliza mmoja wa masahaba zake: unajishughulisha na kazi gani? Sahaba huyo akajibu, kwa sasa nimesimamisha kazi yangu ya biashara. Imam Sadiq AS akamwambia, kwa utaratibu huo mali yako itakwishwa. Usiache kufanya biashara na zitafute fadhila za Mwenyezi Mungu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. http://kiswahili.irib.ir