Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (8)
Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (8)
0 Vote
135 View
Bismillahir Rahmanir Rahim Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Imam Muhammad Baqir AS mmoja wa watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW anasema katika dua moja kwamba: "Ewe Mwenyezi Mungu! Ninakuomba madhali ni hai unijaalie maisha mazuri na ninataka unipatie maisha ambayo yatakuwa sababu ya kunipatia nguvu ya kukutii na kunifanya nipate radhi Zako za peponi." Katika makala yetu iliyopita tulisema kuwa, sira ya Mitume AS na waja wema wa Mwenyezi Mungu inaonyesha jinsi watu hao wa Mwenyezi Mungu walivyolipa umuhimu suala la kazi na kufanya hima kwa ajili ya kujitafutia riziki. Historia inaonyesha kuwa, Mitume wengi walijishughulisha na kazi kama kilimo, kuchunga, biashara na useremala. Katika mantiki ya Uislamu kufanya kazi ni ibada na kama hatua hiyo itaambatana na raghba ya kupata riziki ya halali kwa ajili ya kuendeshea maisha basi ujira na thawabu zake ni sawa na kufanya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume SAW aliwasisitizia watu kwa maneno na vitendo juu ya kufanya kazi na kuwataka wajiepushe na kukaa bila kazi. Maneno yafuatayo ya Bwana Mtume SAW yanayonyesha umuhimu mkubwa wa kufanya kazi kwa mujibu wa Uislamu. Mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema: "Mtu anayefanya kazi na kujituma kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya kimaisha ya familia yake, ni sawa na mtu anayepigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu..." Aidha amesema, ninauhofia umma wangu mambo matatu kuliko mambo mengine nayo ni kuabudu tumbo, kulala sana na kukaa bila kazi..." Katika sehemu nyingine Bwana Mtume SAW anasema: "Mtu ambaye anaweka mzigo wa maisha yake katika mabega ya watu wengine yuko mbali na rehma za Mwenyezi Mungu." Historia ya maisha ya Bwana Mtume SAW inaonyesha kwamba, mbora huyo wa viumbe alianza kufanya hima na kazi tangu akiwa kijana mdogo. Akiwa katika rika la uchipukizi na ujana alikuwa akifanya kazi ya kuchunga mifugo na katika kipindi cha ubarobaro wake alikuwa akifanya kazi ya biashara. Baada ya kubaathiwa na kupewa Utume pia, Muhammad SAW hakuacha kufanya kazi zake na katu hakuishi maisha kama ya Wafalme na mabwanyenye. Jukumu na masuuliya yake ya Utume yalikuwa na mazonge mengi lakini hayakumzuia kufanya kazi zake nyingine zinazohusu maisha yake. Akiwa mjini Madina, Mtume SAW aliitumia sehemu kubwa ya umri wake kwa ajili ya kufikisha risala ya Mwenyezi Mungu na kujihami dhidi ya maadui. Pamoja na hayo yote, hakuacha kutumia hata fursa ndogo aliyoipata kwa ajili ya kufanya kazi na hima kwa ajili ya maisha yake na familia yake. Mtume SAW alikuwa akisema, Mwenyezi Mungu anapenda kumuona mja wake amechoka akiwa katika jitihada za kutafuta riziki ya halali. Katika sehemu moja alipokwa akinong'ona na Mwenyezi Mungu Mtume huyo wa Uislamu anasema: " Ewe Mola! Najikinga Kwako na uvivu na kukaa bila kufanya kazi." Aidha amesema, mtu ambaye ana maji na ardhi lakini akakumbwa na ufukara na umasikini kutokana na kutojishughulisha, basi mtu huyo yuko mbali na rehema za Mwenyezi Mungu." Imekuja katika historia ya maisha ya Bwana Mtume SAW kwamba, alikuwa pamoja tena bega kwa bega na Waislamu wakati wa ujenzi wa msikiti wa Quba na alikuwa akibeba mawe na matofali kama walivyokuwa wakifanya Waislamu wengine. Kila mara mmoja wa masahaba zake alipokuwa akija na kutaka kuifanya kazi iliyokuwa ikifanywa na Mtume huyo ili yeye apumzike, Mtume SAW alikuwa hakubali na alikuwa akisema kumwambia sahaba huyo: We nenda ukachukue jiwe jingine." Hebu sasa na tukizingatie kisa kifuatacho ambacho kina ibra na mafunzo kuhusiana na umuhimu wa kazi. Siku moja Bwana Mtume SAW alimuona kijana shababi mwenye nguvu akiwa anajishughulisha na kazi asubuhi na mapema. Baadhi ya watu waliokuwa wamefuatana na Mtume SAW wakasema: Laiti kijana huyu angetumia nguvu zake za ujana katika njia ya Mwenyezi Mungu, angestahiki mno kusifiwa. Mtume baada ya kusikia maneno yao hayo akasema: Msiseme hivyo, kama kijana huyu anafanya kazi kwa ajili ya kudhamini mahitaji yake na asiwe mhitaji wa mtu mwingine, basi anafanya kazi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Vile vile kama anafanya kazi hii kwa ajili ya baba na mama yake wasio na uwezo au kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya mwanawe na kuwafanya wasiwe wahitaji wa watu wengine, bado atakuwa anafanya kazi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ushahidi wa historia unaonesha kuwa, Bwana Mtume SAW alikuwa akiamini kwamba, zawadi bora kabisa hupatiwa watu wanaojituma na kuhangaika kwa ajili ya kutafuta riziki. Anasema kuwa, "Kila mtu anayekula kutokana na kipato cha halali, milango ya pepo hufunguliwa kwa ajili yake ili aingie peponi kupitia mlango autakao." Moja ya mambo ambayo yanaonekana kuzingitiwa katika maneno na sira ya Bwana Mtume SAW ni elimu na ufahamu wa kazi. Hapana shaka kuwa, mtu anayefanya kazi kwa umahiri na ufahamu mkubwa hupata natija nzuri zaidi ya kazi yake. Kuhusiana na jambo hili, Mtume SAW anamwambia Ibn Mas'oud: "Ewe Ibn Mas'oud, wakati unapojiandaa kwa ajili ya kufanya kazi fulani, ifanyeni kazi hiyo kielimu na kifikra na jiepushe na suala la kufanya kazi bila ya umakini na ufahamu." Katika sira ya Bwana Mtume SAW suala la ustahiki katika kuwachagua watu kwa lengo la kuwakabidhi majukumu na masuuliya ni jambo lililokuwa likipewa umuhimu mkubwa mno. Kwa mtazamo wa Mtume ukubwa wa kidhahiri wa mtu hakikuwa kigezo cha mtu kukabidhiwa maasuuliya na jukumu. Bwana Mtume SAW mbali na imani na taqwa alikuwa akizingatia pia suala la mtu kuwa na ujuzi wa kazi husika anayotaka kumpatia. Kwa mfano wakati Bwana Mtume SAW anamchagua Utab bin Aseer kuwa Gavana wa Makka alimwambia: " Kama ningekuwa namfahamu mtu mwingine aliyebora kuliko wewe, ningemteua.' Kwa muktadha huo, tunafahamu kwamba, suala la kumchagua mtu anayestahiki kwa ajili ya kuchukua jukumu fulani ni jambo ambalo nalo lilikuwa likipewa umuhimu mno na Bwana Mtume SAW. Hii leo hali iko kinyume kabisa hasa katika tawala za kifalme ambapo tunaona mtu anapewa jukumu la uongozi fulani kwa kuwa anatoka katika familia ya mfalme au anateuliwa kushika wadhifa fulani kutokana na urafiki na ukuruba alionao na kiongozi fulani wa ngazi za juu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. http://kiswahili.irib.ir