Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (6)
Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (6)
0 Vote
97 View
Bismillahi Rahmanir Rahim Kazi ni taklifu na jukumu ambalo mfumo wa ulimwengu umeliweka katika mabega na dhima ya mwanadamu ili mja huyu aweze kudhamini mahitaji yake ya kimaisha kupitia hima na idili yake. Hima na jitihada na harakati za maisha zilianza tangu mwanzo tu wakati Nabii Adam AS alipoumbwa na Mwenyezi Mungu na kuwekwa katika mgongo wa ardhi. Hata hivyo suala hilo halihusiani na mwanadamu tu bali viumbe wote wamo katika hali ya harakati ha hima ili waweze kudhamini chakula na mahitaji yao kimaumbile na hivyo kuweza kubakia hai. Hata mnyama wa porini hana budi kutembea huku na huko msituni ili kutafuta nyasi au kitoweo. Kama tulivyosema, hima na kufanya kazi katika mtazamo wa Uislamu ni jambo ambalo lina nafasi maalumu. Hii inatokana na kuwa, jambo hili lina sudi na faida nyingi za kimaada na kimaanawi kwa mwanadamu. Kupitia aya za Qur'ani Tukufu na mafundisho ya dini inapatikana natija hii kwamba, mwanadamu anapaswa kupiga hatua katika njia ya ustawi na kukwea kimaada na kimaanawi katika kivuli cha akili, tadbiri, mipango, hima na idili. Kufanya kazi na kuwa na hima na juhudi kwa ajili ya kutafuta riziki ya halali mbali na kufukuza uvivu na hali ya kukata tamaa katika ujudi wa mtu, hatua hiyo huleta nishati na uchagamfu. Kazi ni wenzo bora kabisa kwa ajili ya kuishughulisha kwa salama fikra na mwili wa mwanadamu. Wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, chimbuko kuu la ushindi ni hima na juhudi za wanadamu na watu ambao wanafanya hima na juhudi zaidi huwa ni wenye saada na mafanikio zaidi na wale ambao wana uvivu na ambao hawafanyi hima hukosa mafanikio na hivyo kutofikia saada na ufanisi. Ndio maana wahenga wakasema, uvivu ni adui mkubwa wa maendeleo. Akili inahukumu kwamba, ili mwanadamu ajikomboe na kuondokana na umasikini anahitajia kufanya kazi na hivyo kuweza kudhamini hawaiji na mahitaji yake ya maisha kwa njia ya izza na heshima; badala ya kujidhalilisha na kujidunisha kwa kuwa ombaomba mbele za watu. Nukta ya kuzingatia kuhusiana na mafundisho ya Uislamu ni kuwa, dini hii ya Mwenyezi Mungu imekokoteza na kuusia mno juu ya kufanya kufanya kazi na kuwa na hima sambamba na kuwa na taqwa na uchaji Mungu. Kwa maana kwamba, wakati mtu anapofanya kazi ya kutafuta riziki yake halali anapaswa kutomsahau Mwenyezi Mungu na kutoacha kushikamana na taqwa na uchaji Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 37 ya Surat Nur kwamba: Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Katika aya hii Allah anataka kuonyesha kuwa, watu ambao ni wa Mwenyezi Mungu yaani watu ambao wameshikamana na taqwa na uchaji Mungu, kujihusisha kwao na biashara na kazi za kutafuta riziki kwa ajili ya kudhamini mahitaji yao ya maisha huwa hakuwashughulishi kiasi cha kuwafanya waghafilike na suala la kumtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kuwa, watu hao humfanya Mwenyezi Mungu kuwa mhimili mkuu katika maisha yao ambapo juhudi za kimaada na kiuchumi hazipaswi kumfanya mtu amsahau Mwenyezi Mungu bali anapaswa kumtanguliza Allah katika kazi zake hizo. Kwa muktadha huo kazi ya kiuchumi na hima ya kutafuta riziki inapaswa kuathiriwa na kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kuchunga taqwa. Kwa maana kwamba, mtu anapokuwa katika pirika pirika za kutafuta riziki hapaswi kumuasi Mwenyezi Mungu. Kama anga ya kiuchumi inayotawala katika jamii itakuwa ni kujiepusha na kumuasi Mwenyezi Mungu, kufanya mambo kwa usahihi na ushirikiano, bila shaka jamii kama hiyo itakuwa na mahusiano salama baina ya wanajamii. Kwa upande mwingine, wakati wanadamu wanapomuogopa Mwenyezi Mungu na kuchunga taqwa, hujiepusha na kazi za haramu na zile ambazo haziko katika ridhaa ya Mwenyezi Mungu. Hatua hiyo hupelekea kushuka zaidi rehema na baraka za Mwenyezi Mungu. Allah anasema katika aya za 2 na 3 za Surat Talaq; "...Na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea. Na humruzuku kwa jiha asiyotazamia...." Kwa hakika waja wema wa Mwenyezi Mungu wanapokuwa wanafanya kazi yoyote ile na harakati yoyote ile wanayojishughulisha nayo, awali kabisa hupiga hatua kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na humfanya Allah kuwa msimamizi wa kazi na miamala yao katika kila hali. Ni kwa msingi huo ndio maana kazi na hima kwa ajili ya kutafuta pato la kudhamini maisha kwa namna fulani inahesabiwa kuwa ni aina ya ibada. Imam Muhammad Baqir AS mmoja wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW ansema akinukuu kutoka kwa Mtume SAW ya kwamba amesema: "Ibada ina vigawanyo sabini ambapo kigawanyo chake bora kabisa ni hima na kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta riziki ya halali." Ni kutokana na uhakika huo ndio maana kazi na kufanya hima ambako kunafanywa na mtu kwa ajili ya kudhamini mahitaji yake ya maisha na ya familia yake, mbali na kupelekea ustawi na uboreshaji maisha ya walimwengu, kazi hiyo inaweza kuwa sababu ya ujira na thawabu kwa ajili ya kesho akhera. Ndio maana imekuja katika riwaya na hadithi kwamba, dunia ni konde la akhera. Bila shaka shamba hili litastawi na kutoa mazao bora kwa kuweko hima na juhudi bora zinazoambatana na kufanya mambo mema na kumcha Mwenyezi Mungu. Sira na maneno ya Mitume na waja wema wateule wa Mwenyezi Mungu yanaonyesha kwamba, maisha ya watukufu hao yalichanganyika na kazi na kufanya hima na kwamba, cheo chao cha kuwa wao ni Mitume wateule wa Mwenyezi Mungu hakikuwazuia kufanya mambo yao ya binafsi na kazi za kimaisha. Tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa kusema kuwa, ili mwanadamu aweze kuendelea na maisha na hata aweze kuboresha maisha yake sambamba na kukidhi mahitaji yake ya kila siku ya kimaisha anahitajia kufanya kazi na kujituma katika kutafuta maisha. Hakuna matumaini na ndoto alizonazo mwanadamu ambazo zinaweza kufikiwa na kutimia pasina ya kuweko hima na juhudi mtawalia katika maisha. Kila mtu au taifa ambalo linataka kufikia katika vilele vya maendeleo na mafanikio na hivyo kuvuka vizingiti na vikwazo vyote vilivyoko katika njia hiyo na kuyafikia mafanikio, ni lazima lijiepusha na uvivu na kutaka kupata mambo bure bure na kirahisi pasina ya kujituma na kufanya hima. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. http://kiswahili.irib.ir