Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (11)
Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (11)
0 Vote
97 View
Moja ya masuala muhimu katika mahusiano ya kiuchumi na kijamii ni kwamba, wanadamu wanalazimika kustafidi na kazi na huduma za kila mmoja. Kwa maana kwamba, kila mmoja anamtegemea mwenzake katika shughuli zake iwe ni za kiuchumi, kibiashara, kijamii na kadhalika. Hapana shaka kuwa, gurudumu la maisha ya mwanadamu linategemea ushirikiano, huduma za pamoja na kila mtu kustafidi na kazi ya mwenziwe na hakuna mtu ambaye anaweza kujigamba kwamba, anaweza kuendesha maisha yake pasina ya kumtegemea mtu mwingine katika jamii. Imam Ali bin Abi Talib AS anasem a kuhusiana na suala hili kwamba: "Hakuna mwanaadamu ambaye anaweza kufanya kazi zake mwenyewe pasina ya kumtegemea mwenzake kama ujenzi, useremala na kadhalika." Hii ni kusema kwamba, kila mmoja anamtegemea mwenzake. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana ikaelezwa kwamba, hupaswi kuidharua kazi ya mwenzio na kuiona duni, madhali kazi hiyo ni utoaji huduma kwa jamii. Hata kazi za usafishaji barabara au ukusanyaji wa taka na maji chafu katika jamii ambazo kikawaida hufanywa na wafanyakazi wa manispaa za miji ambazo yamini zikaonekana duni na baadhi ya wenye fikra finyu, ni kazi zenye thamani kubwa kwa jamii. Kwani kama leo wafanyakazi hao watagoma, bila shaka mji hautokalika kwa uchafu na takataka. Hapana shaka kuwa, kama wanadamu katika jamii watakuwa na kiwango sawa cha kimaisha yaani wawe katika daraja moja, msingi wa ushirikiano baina yao utatetereka kama sio kusambaratika kabisa. Kwani kama wanadamu watakuwa na uwezo sawa na unaolingana kutakuwa hakuna haja ya mtu kumhitajia mwenziwe na natija ya hilo ni kutokuwa na maana suala la ushirikiano wa kijamii na kiuchumi. Kama ambavyo kama seli za mwili wa mwanaadamu zingekuwa zinasha bihiana kwa upande wa kukabiliana na mambo, mfumo wa mwili ungevurugika. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana kila seli za mwili zina muundo wake na kazi yake maalumu katika mwili wa mwanadamu kazi ambayo haiwezi kufanywa na seli nyingine za mwili. Ukweli wa mambo ni kuwa, kila kundi miongoni mwa wanadamu lina suhula, uwezo na kipaji cha kufanya kazi maalumu ambapo linaweza kuwapatia watu wengine suhula na ujuzi huo. Kuhusiana na kugawanywa majukumu baina ya watu, Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 32 ya Sura ya Zukhruf kwamba: "Kwani wao ndio wanaogawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya." Hata hivyo kuweko kwa tofauti hizi katika jamii, haipaswi kuwa kisingizio cha kundi fulani kulinyonya kundi jengine na ndio maana katika Uislamu kukaweko na sheria na kanuni za kijamii kwa ajili ya kulinda na kutetea haki za wafanyakazi na pamoja na suala la ajira kwa ujumla. Katika aya mbalimbali Qur'ani Tukufu inaashiria suala la kazi, ajira na kuajiri nguvu kazi. Mfano wa wazi ni kisa cha Nabii Mussa na Shu'aib katika Sura ya al Qasas au kisa cha Nabii Mussa na Khidhr katika sura ya Kahf. Au pendekezo alilopatiwa Dhul Qarnain la kujenga kizuizi na ukuta ili mkabala na kazi hiyo apate ujira. Hivyo basi suala la kufanya kazi na kupata ujira halikuanza leo wala jana bali lilikuwako tangu enzi na dahari. Kwa mujibu wa sheria za kazi, mfanyakazi ni mtu ambaye anapokea ujira, mshahara, posho na kadhalika mkabala na kutekeleza takwa la mwajiri wake au kazi aliyopatiwa aifanye. Kwa hakika wafanyakazi ni tabaka lenye thamani kubwa zaidi katika jamii hasa kwa kutilia maanani kwamba, sehemu kubwa ya gurudumu la uchumi imo katika mikono yenye nguvu ya wafanyakazi hao. Kimsingi kazi ya wafanyakazi hutekeleza sambamba na kurahisisha mipango ya uchumi ya serikali na hivyo kupelekea kuweko uzaishaji wa utajiri na kustawi uchumi katika jamii. Msukumo mkubwa na muhimu kabisa wa watu kufanya hima na kazi ni kupata ujira na mshahara. Mishahara wanayopata watu huitumia kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya kimaisha pamoja na familia zao. Waajiri wana jukumu la kuwalipa wafanyakazi mishahara na ujira unaostahiki na hivyo kuwandaalia mazingira mazuri kisaikolojia kwa kujaribu kuboresha maisha yao. Hatua hiyo huwafanya watu kuwa na hamu na shauku zaidi ya kufanya kazi vizuri zaidi na zaidi. Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume SAW ya kwamba amesema: "Kadiri mwanadamu atakavyoweza kuandaa suhula za maisha kwa kadiri ya mahitaji yake, ndivyo ambavyo huwa na utulivu wa kisaikolojia." Kwa mtazamo wa Uislamu uhusiano wa mfanyakazi na mwajiri ni uhusiano wa washirika wawili. Aidha kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu muamala wa pande mbili wa mwajiri na mfanyakazi wake unapaswa kuwa wenye huba, ushirikiano, kuaminiana na kuheshimiana. Muamala wa mfanyakazi na mwajiri au tajiri haupaswi kuwa muamala wa mtumwa na Bwana wake. Mtume SAW, Imam Ali AS na Maimamu watoharifu daima walikuwa wakiwathamini wafanyakazi na walifanya hima kutetea haki zao. Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema: "Haki ya mfanyakazi kwa mwajiri wake ni mwajiri wake kumpatia mfanyakazi huyo mavazi mazuri na chakula na kutomfanyisha kazi kuliko uwezo wake." Aidha mbora huyo wa viumbe amenukuliwa katika sehemu nyingine akisema kwamba: "Nyinyi nyote mna masuuliya kwa wafanyakazi na walioko chini yenu. Mtu yeyote ambaye atadhulumu katika kumpatia mfanyakazi ujira wake, Mwenyezi Mungu atazitokomeza amali zake nzuri na kumnyima harufu itulizayo moyo ya peponi" (yaani hatomuingiza peponi). Imam Sajjad AS anasisitiza katika risala yake ya haki maarufu kwa jina la Risalatul Huquq juu ya kuchunga uadilifu na kuwa na upole kwa wafanyakazi na vile vile kufumbia macho makosa yao. Tunahitimisha makala hii kwa kukunukulieni baadhi ya semi za Ayatollah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Akihutubia kwa mnasaba wa Mei Mosi, yaani siku ya wafanyakazi mwaka 2010, Ayatullah Khamenei alisema, mfanyakazi akiwa nyuma ya mashine ya kufanyia kazi au akiwa anajishughulisha na kupanga na kubuni kitu, au akiwa anajishughulisha na kazi yake shambani au popote alipo katika kazi ya uzalishaji na kuleta mazao, anapaswa kuhisi kwamba, anafanya kazi kubwa, muhimu na yenye thamani. Aidha akizungumzia nafasi muhimu ya wafanyakazi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema: Tabaka la wafanyakazi kwa hakika ni tabaka ambalo liko mstari wa mbele katika juhudi za pamoja za nchi na taifa kwa ajili ya kujenga taifa na kusukuma mbele kurudumu la maendeleo. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Na Salum Bendera http://kiswahili.irib.ir